IQNA

Sayyid Nasrallah: Vita dhidi ya Iran vitasababisha mlipuko mkubwa Asia Magharibi

22:15 - February 09, 2022
Habari ID: 3474909
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Nasrallah ameonya kuwa vita vyovyote dhidi ya Iran vitasababisha mlipuko mkubwa katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Ameongeza kwamba kipaumbele cha Marekani kwa sasa si vita na Iran bali ni makabiliano na Russia na China. Amesema Iran imeazimia ipasavyo kujibu tishio lolote na haifanyi mzaha na yeyote.

Akizungumza Jumanne usiku na televisheni ya Al-Alam, Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Chama cha Hizbullah amesema kwamba hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukuliwa kama mfano bora wa kuigwa na mataifa mengine duniani, kutokana na siasa zake imara za kuijitawala na kutoruhusu kutawaliwa au kuathiriwa na madola ya kigeni.

Sayyid Nasrallah amesema katika utawala wa kifalme wa Shah Iran ilikuwa ikitawaliwa kikamilifu na Marekani lakini baada ya ushindi wa Mpainduzi ya Kiislamu na kupinduliwa utawala wa Shah, utawala huo wa Wamarekani ulifikia kikomo na pia washirika wao wa karibu yaani utawala wa kigaidi wa Israel wakawa wamefukuzwa Iran.

Amesisitiza kwamba Iran ni nguvu kubwa katika eneo na kwamba njama zozote za kuanzisha vita dhidi yake zitapelekea kulipuka eneo lote hili nyeti katika ramani ya dunia.

Amesema siasa za Marekani zimejengeka kwenye misingi ya ubabe na uchokozi dhidi ya mataifa mengine kama tunavyoona ikafanya hivi sasa dhidi ya Russia na China.

Amesema katika sehemu nyingine ya mahojiano yake hayo na televisheni ya Al-Alam kwamba moja ya sababu za uchokozi na uhasama wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa nchi hii inaongozwa na kiongozi shupavu, mwenye fikra huru na shujaa ambaye haruhusu hata kidogo utajiri na maliasili za taifa lake kuporwa na wageni.

Katibu Mkuu wa Chama cha Hizbullah cha nchini Lebanon ameashiria furaha kubwa waliyokuwanayo wananchi wa Iran wakati wa kurejea nchini Imam Khomeini (MA) kutoka uhamishoni na kusema hiyo ni moja ya nukta za kuvutia zaidi katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanayojulikana kama Alfajiri Kumi.

Amesema mapinduzi hayo yameipelekea Iran kuwa nguvu kubwa zaidi katika eneo zima la Asia Magharibi  na ambayo ina taathira kubwa si tu katika matukio ya kieneo bali katika ulimwengu mzima.

Tarehe 12 Bahman sawa na tarehe Mosi Februari 1979 na baada ya kulazimika kuishi uhamisho kwa miaka 15, hatimaye Imam Khomeini (MA) aliwasili na kulakiwa nchini na umati mkubwa wa wananchi wa Iran. Siku kumi baada ya kuwasili kwake nchini, yaani tarehe 22 Bahman 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Iran, sawa na tarehe 11 Februari Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalifikia ushindi ambao uliasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa msingi huo kipindi cha kati ya kuwasili nchini Imam Khomeini na kutangazwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hujulikana kama Alfajiri Kumi.

Sehemu nyingine ya mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrullah na televisheni ya al Alam inahusiana na kadhia ya kuchora na kuainisha mipaka ya majini ya Lebanon na utawala haramu wa Israel kwa upatanishi wa Marekani na Umoja wa Mataifa. Amesema: "Hizbullah haiingilii suala la kuainisha mipaka na jambo hilo linaihusu serikali ya Lebanon. Hata hivyo Hizbullah inatoa sharti moja kuu nalo ni kwamba suala hilo lisitumiwe kama chombo cha kuanzisha uhusiano na ushirikiano na adui Mzayuni."

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameashiria sherehe zinazoendelea hapa nchini za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kusema: Siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni miongoni mwa siku adhimu za Mwenyezi Mungu. Iran ni mfano wa kuigwa wa nchi inayojitawala na yenye uhuru kamili ambako wananchi wanawachagua wawakilishi wao; wakati nchi nyingi za Magharibi mwa Asia zinazodai kuwa huru na kujitawala ni tegemezi kwa balozi za nchi ajnabi."

/4034980/

captcha