IQNA

Ismail Hania wa Hamas amtumia ujumbe Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu

10:19 - February 15, 2022
Habari ID: 3474932
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati wa Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amemtumia salamu na ujumbe maalumu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kumshukuru kwa misimamo yake ya kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Ijumaa ya tarehe 22 Bahman 1400 iliyosadifiana na Februari 11, 2022, ilikuwa siku ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambayo yalipata ushindi kamili tarehe 11 Februari 1979 kwa uongozi wa Imam Khomeini (MA). 

Kwa mujibu wa shirika la habari la al-Mayadeen, Ismail Hania, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, amebainisha katika ujumbe wake huo kwa Ayatullah Khamenei kuwa: ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa ni matunda makubwa kwa vuguvugu la Muqawama wa Kiislamu.

Katika ujumbe wake huo, Hania amemhutubu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akisema: harakati ya Hamas na wananchi wa Palestina wako pamoja na wewe katika kusherehekea mnasaba huu wa furaha ili kubainisha pongezi na shukrani zao za dhati kutokana misimamo yako adhimu na ya kudumu ya kusimama imara pamoja na Palestina, malengo yao matukufu, na uungaji mkono wako kwa watu wa nchi hii na muqawama wao wa kishujaa katika kutetea na kupigania haki zao za kisheria.

Aidha, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesisitiza kuwa harakati hiyo ina imani na matumaini ya kuendelezwa misimamo hiyo na kuendelea kutolewa michango katika kufanikisha ushindi wa Palestina na uungaji mkono kwa watu wake na mkakati wao wa muqawama, licha ya hatari na changamoto mbalimbali zinazoyakabili malengo matukufu ya Palestina.

4036507/

captcha