Huku akilaani mauaji ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Masoud Pezieshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter): Mshikamano kati ya mataifa mawili yenye fahari ya Iran na Palestina utakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali, na njia ya muqawama na kutetea wanaokandamizwa itakuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italinda ukamilifu ardhi yake, izza, na heshima yake, na wavamizi wa kigaidi watajutia kitendo chao cha woga walichokifanya.
Naye
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kuutaka ujiandae kwa matokeo mabaya na majibu makali ya kuumiza kwa kumuua kigaidi Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS).
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh ameuhutubu utawala katili wa Israel kwa kuuambia, "Muwe tayari kuwafanya Wazayuni waelewe adhabu kali inayowasubiri kwa kumwaga damu ya mgeni ndani ya ardhi yetu."
Ismail Haniya na mmoja wa walinzi wake wameuawa shahidi usiku wa kuamkia leo baada ya kushambuliwa makazi yao hapa mjini Tehran, saa chache baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.
Wakati huo huo, Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imesisitiza pia kuwa, hakuna shaka utawala wa Kizayuni utakabiliwa na jibu kali, zito na la kuumiza kwa kitendo chake cha kumuua shahidi Ismail Haniyah.
Taarifa ya IRGC imebainisha kuwa: Mauaji ya kigaidi ya Haniyah yatakabiliwa na jibu kali na la kuumiza kutoka kwa Mrengo wa Muqawama hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
4229274