IQNA

Kadhia ya Palestina

Kiongozi Muadhamu : Bendera ya juu kabisa ya Uislamu leo iko mikononi mwa watu wa Gaza

20:37 - July 30, 2024
Habari ID: 3479202
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza ushujaa wa wananchi wanaodhulumiwa na wenye nguvu wa Ghaza na kusema: Leo bendera ya juu kabisa ya Uislamu iko mikononi mwa watu wa Ukanda wa Gaza.

Akizungumza leo Jumanne ofisini kwake na Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na Ziad al-Nakhaleh, Katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Palestina, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu msimamo na muqawama usio na kifani wa watu wanaodhulumiwa wa Gaza na kusema: Leo hii bendera ya juu kabisa ya Uislamu iko mikononi mwa wananchi wa Palestina na watu wa Gaza na mapambano yao yameandaa uwanja wa kuimarishwa zaidi Uislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameorodhesha daghadagha za siku zote za wanafikra wa Kiislamu kuwa ni pamoja na jinsi ya kuuneza Uislamu na kuweka kigezo cha kuigwa na jamii ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Mwenendo unaoongezeka hii leo wa Uislamu kuwavutia wengi duniani ni ishara inayoonyesha ukubwa wa mapambano ya taifa la Palestina na watu wa Gaza.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Sababu kuu ya utukufu wa muqawama ni wananchi wa Gaza na wakaazi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kwamba inatarajiwa kuwa taifa la Palestina na vikosi vya muqawama vitapata ushindi wa mwisho kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu.

Akipongeza kuchaguliwa rais mpya wa Iran, Ismail Haniyeh amesema uchaguzi wa hivi karibuni wa Iran ni dhihirisho la demokrasia yenye msingi wa fikra za Kiislamu na kuongeza kuwa katika kikao chake cha karibuni na Masoud Pezeshkian, rais mpya wa Iran, alihisi kwa karibu na kwa mara nyingine tena, misimamo imara na ya dhabiti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na suala zima la kutetea Palestina na harakati ya muqawama, na kuwa wananchi wa Palestina wanajifaharisha na misimamo hii ya kuvutia.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas pia amefafanua hali ya hivi sasa ya kisiasa huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusema: Jana ilikuwa siku ya 300 ya vita vya Gaza na muqawama umefikia hatua muhimu na ya kihistoria ambapo wananchi wa Palestina na wapiganaji wa muqawama wanapasa kuimarisha ushujaa na ushindi wao.

Ziad al-Nakhaleh, Katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Palestina amepongeza kuchaguliwa Rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian na kusifu misimamo yake ya kuunga mkono Palestina na muqawama na kusema: Kuwepo kwa wakati mmoja viongozi wa Hamas na Jihad Islami mjini Tehran ni ishara na nembo ya umoja wa vikosi vya muqawama huko Palestina, na kutokana na umoja huu, uratibu na ushirikiano katika mrengo wa muqawama katika eneo pia uko kwenye kiwango bora zaidi.

3489305

Habari zinazohusiana
captcha