IQNA

Fainali ya Mashindano ya 38 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran

9:57 - February 27, 2022
Habari ID: 3474983
TEHRAN (IQNA)- Mkuu wa Idara ya masuala ya Qur'ani ya Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri amesema maandalizi ya mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani yanayofanyika kila mwaka mjini Tehran yamekamilika.

Majidi Mehr, ameeleza hayo katika kikao na waandishi habari na kufafanua kuwa, mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani tukufu yataanza siku ya Jumatatu ya tarehe 28 Februari na kuendelea hadi tarehe 5 Machi.

Amesema katika mashindano ya mwaka huu washiriki 190 kutoka nchi 69 wameshiriki katika mashindano ya mchujo yaliyofanyika kwa njia ya intaneti. Baada ya uchunguzi uliofanywa na jopo la majaji, washiriki 62 kutoka nchi 29 walifanikiwa kuingia fainali.

Amesema fainali za mashindano hayo zitaanza rasmi Jumatatu Februari 28 na kuendelea hadi Machi 5 ambapo baadhi watashiriki kwa njia ya intaneti.

Nara na kaulimbiu ya mashindano ya mwaka huu imetajwa kuwa ni "Kitabu Kimoja Umma Mmoja."

Mkuu wa Idara ya masuala ya Qur'ani ya Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri amebainisha kuwa, usomaji wa tajwidi, tartili na kuhifadhi Qur'ani yote kwa washiriki wanawake na wanaume ni miongoni mwa vitengo vya mashindano ya mwaka huu na akaongeza kwamba, sambamba na mashindano ya 38 ya kimataifa ya Qur'ani tukufu, yatafanyika pia mashindano ya saba ya Qur'ani kwa wanafunzi wa skuli za nchi za Ulimwengu wa Kiislamu na vilevile mashindano ya tano ya Qur'ani katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa washiriki wenye ulemavu wa macho.

Wawakilishi wa Tanzania, Kenya, Uganda ni miongoni mwa walioingia fainali za mashindano ya Qur'ani mwaka huu nchini Iran.

4038889

captcha