IQNA

Utamaduni

Yemen, mgeni maalumu katika Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran

22:55 - May 12, 2024
Habari ID: 3478808
IQNA - Yemen inashiriki katika Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran kama mgeni rasmi kwa lengo la kuimarisha utamaduni wa muqawama au mapambano ya Kiislamu.

"Kushiriki kwetu katika maonyesho haya ya vitabu ni hatua ya kuanzisha mwanzo thabiti, imara, na endelevu kuelekea ushirikiano wa kitamaduni katika nyanja zote za mapambano Kiislamu," Abdurrahman Murad, mkuu wa Shirika la Vitabu la Yemen, aliiambia IQNA siku ya Ijumaa.

Maonesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran (TIBF) yalizinduliwa Jumatano ambapo yanashirikisha  zaidi ya wachapishaji 2,500 wa Iran na 60 wa kigeni.

Yemen imepewa hadhi ya  mgeni maalum katika maonyesho hayo  ya vitabu mwaka huu. Hapo awali, India ilipangwa kuwa mgeni maalum, lakini vikwazo vya kusafiri kwa raia wa India kuja Iran vilisababisha waandaaji kualika Yemen badala yake.

Murad aliangazia historia tajiri ya Yemen na ushawishi wake mkubwa kwa ustaarabu wa Mashariki ya Kati na Waarabu, na vile vile uhusiano wa kitamaduni na kibiashara wa taifa hilo na Iran, ambao umekuwepo kwa milenia.

“Mshikamano wa kina baina ya watu wa Yemen na Iran umejikita katika imani yao ya pamoja ya Kiislamu, alisema, na kuongeza kuwa uhusiano huu unaimarishwa na heshima ya watu wa mataifa mawili kwa Mtukufu Mtume (SAW), Qur’ani Tukufu, Imam Ali (AS), Imam. Hasan (AS), na Imam Hussein (AS)."

 

Akielezea furaha yake ya kuwa mgeni maalum katika Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran, Murad alibainisha kuwa licha ya mzozo unaoendelea, uchapishaji bado ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kitamaduni na ustaarabu wa Yemen. Alisema kuwa karibu vitabu 600 huchapishwa nchini Yemen kila mwaka.

Akizungumzia hali ya maktaba za umma nchini Yemen, Murad alibaini kuwa kuna takriban maktaba 100 za umma na za kibinafsi nchini humo, huku nyingi zikiwa katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a. Hata hivyo, vita ambavyo Yemen imepitia kwa miaka mingi vimesababisha kufungwa kwa takriban maktaba 40, aliongeza.

Amesisitiza kuwa licha ya uhaba wa maktaba nchini Yemen, zile zilizopo zina utajiri mkubwa wa rasilimali zinazohusisha nyanja za kiuchumi, kihistoria, kisiasa, kijamii na kifasihi.

Alisisitiza zaidi kwamba sehemu kubwa ya hazina za maktaba ya Yemen ni vitabu vya kali ambavyo ni karibu 48,000.

Alipoulizwa kuhusu lengo lake kuu la kuhudhuria Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran, Murad alisema kuwa haikuwa tu kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kupanua maingiliano ya kiutamaduni na kisanii kati ya Iran na Yemen, bali pia ni kuonyesha asili ya kupenda amani, na ukarimu ambao ni muhimu kwa utamaduni wa Yemeni."

Murad aliongeza kwamba, kutokana na mzingiro na vita vinavyoendelea, haikuwezekana kuleta vitabu zaidi kutoka Yemen. Hata hivyo, alihakikisha kwamba nyenzo zilizoonyeshwa kwenye kibanda cha Yemen hutoa muhtasari wa vitabu vinavyopatikana, shughuli za uchapishaji, na mandhari ya jumla ya fasihi nchini Yemen.

TIBF, ikiwa ni maonyesho kuu ya biashara ya vitabu nchini Iran, yamebadilika na kuwa maonyesho muhimu ya vitabu huko Asia Magharibi baada ya kuandaa matoleo 34 kwa mafanikio. Kila mwaka, maonyesho hayo huvutia mamilioni ya wageni, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi wa vyuo vikuu, wasomi na familia.

Hivi sasa, maonyesho hayo yanatajwa kuwa tukio maarufu zaidi la kitamaduni nchini Iran. Wachapishaji wa kigeni wamewasilisha vitabu kwa lugha za Kiingereza au Kiarabu, Kifaransa, Kijerumani, Kichina, Kikorea na Kijapani

Maonyesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu "Tusome na Tuunde." Maonyesho ya 35 ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran na yataendelea hadi Mei 18 jijini  Tehran katika Eneo la Sala (Musalla) la Imam Khomeini.

3488288

Habari zinazohusiana
captcha