IQNA

Umoja wa Afrika walaani jinai za Israel, UN yataka uchunguzi

18:19 - April 23, 2022
Habari ID: 3475160
TEHRAN (IQNA)- Umoja wa Afrika umelaani hujuma za utawala haramu wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds (Jerusalem) na Ukanda wa Gaa sambamba na kusisitiza uungajo mkono wake kwa watu wa Palestina.

Palestina kwa mara nyingine inashuhudia jinai zinazotekelezwa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina. Kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, Wazayuni wamezidisha ukandamizaji na hujuma zao dhidi ya Wapalestina wanaofika katika msikiti huo mtakatifu kwa ajili ya kufanya ibada zao katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Ijumaa iliyopita, Wazayuni walifanya shambulio kali katika msikiti wa al-Aqsa ambapo waliwajeruhi Wapalestina zaidi ya 450 na kuwakamata wengine 400. Hujuma hiyo pia imekuwa ikiendelea katika siku za karibuni ambapo makumi ya Wapalestina wamejeruhiwa.

Kufuatia hali hiyo, Mohammad Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa taarifa na kulaani hujuma ya askari wa utawala wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na waumini wanaoswali hapo katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.  Moussa Faki pia amelaani hujuma za mara kwa mara za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema   utawala wa Kizayuni wa Israel umekiuka sheria za kimataifa kwa kutumia wanajeshi wake katika kuwatimua Wapalestina kutoka katika nyumba zao.

Moussa Faki pia amesema Umoja wa Afrika utaendelea kuunga mkono Wapalestina.

Wakati huo huo, Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi kuhusiana na mashambulio ya kikatili ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya waumini wa Kipalestina waliokuwa wakifanya ibada katika Msikiti wa Al-Aqsa.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) amesema katika mkutano mjini Geneva kwamba mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa Al-Aqsa huko Quds Mashariki (Jerusalem) yamejeruhi watu 180 wakiwemo watoto 27 kuanzia Aprili 15 hadi 17.

Msemaji wa OCHA ameongeza kuwa: "Lazima kufanyike uchunguzi wa haraka, usioegemea upande wowote, huru na wa wazi kuhusu mashambulizi ya askari wa Israel ambayo yamejeruhi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Al-Aqsa, na wale waliohusika lazima wawajibishwe."

Mji wa Quds ambao una Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu, ni mji mkuu wa nchi ya Palestina na hilo halina shaka hata kidogo na wala mji huo hauwezi kamwe kutenganishwa na ardhi nyingine za Palestina. Msikiti wa Al Aqsa ni moja kati ya maeneo matatu matakatifu zaidi katika Uislamu.

4051536

captcha