IQNA

Rais wa Iran: Mujahidina wataamua hatima ya Palestina

18:12 - April 23, 2022
Habari ID: 3475159
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa: Hii leo, hatima ya Palestina itaamuliwa kwa matakwa na irada ya Mujahidina.

Sayyid Ebrahim Raisi, ambaye usiku wa kuamkia leo amehutubia mkusanyiko wa waumini walioshiriki katika ibada ya usiku wa pili wa Lailatul Qadr katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na waombolezaji wa tukio la kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) mjini Tehran, amesema, wakati moja ilifikiriwa kwamba hatima ya watu wa Palestina ingeamuliwa kwenye meza ya mazungumzo lakini leo, hatima ya Palestina iko mikononi na kwenye irada ya wapiganji wa Jihadi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: "Leo tunashuhudia jinai zinazoshabihiana na za Daesh za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Waislamu na waumini wanaodhulumiwa katika Msikiti wa Al-Aqsa na katika misikiti ya Afghanistan."

Raisi amesema watawala wa Afghanistan wana jukumu la kulinda maisha ya Waislamu wa nchi hiyo wanaouawa shahidi misikitini wakiwa katika ibada ya funga. 

Akizungumzia ujio wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa: Umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu ambao ni moja ya nembo za Siku ya Quds unaongezeka siku baada ya siku kutokana na ikhlasi ya Imam Ruhullah Khomeini, na tunatumai kwamba mshikamano na umoja huo utapelekea kukombolewa Quds na kuwaweesha Wapalestina kupata haki yao wanayoipigania kwa miaka 70.

Miaka 43 iliyopita, Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds.

135868

captcha