IQNA

Sayyid Nasrallah: Hizbullah itajibu papo hapo shambulizi lolote la Israel

16:51 - April 30, 2022
Habari ID: 3475187
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo hautaizuia harakati hiyo kujibu shambulio lolote la utawala bandia wa Israel, akisisitiza kuwa Hizbullah itajibu papo hapo shambulio lolote la utawala huo haramu.

Akizungumza jana kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah alisema kuwa muqawama wa Lebanon uko kwenye kilele cha utayarifu na kwamba iwapo kosa dogo litafanywa na adui Mzayuni, litakabiliwa na majibu ya haraka na ya moja kwa moja.

Sayyid Nasrallah amesema: "Hatutaisahau Palestina" na kuongeza kuwa "suala la Palestina ni sehemu ya dini, imani na heshima yetu". 

Akisisitiza kwamba mchakato wa kuhalalisha uhusiano na utawala wa Kizayuni ni lazima upingwe na kupigwa vita, Katibu Mkuu wa Hizbullah ameeleza kuwa, unafiki mkubwa tunaoushuhudia siku hizi ni kwamba nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi zinadai kuwa suala la kuanzisha uhusiano na Israel ni kuwatumikia wananchi wa Palestina!

Sayyid Nasrallah amesema: Siku moja tutaswali ndani ya Quds na kuisisitiza kwamba: "Wazayuni na maadui wanaiona siku hiyo kuwa iko mbali lakini sisi tunaiona kuwa iko karibu sana".

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameashiria tamko la jana la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kuhusu Quds na kusema tamko hilo linaonyesha dhamira kubwa na thabiti ya kuunga mkono na kuitetea Palestina na harakati za mapambano katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Katika ujumbe wake wa jana kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba madhali utawala ghasibu na mtenda jinai wa Israel unaendelea kuikalia Quds kwa mabavu, kila siku ya mwaka inapaswa kutambuliwa kuwa ni Siku ya Quds. Amesema: Quds Tukufu ni moyo wa Palestina, na nchi yote iliyonyakuliwa ya Palestina kuanzia Bahari ya Mediterania hadi Mto Jordan ni mwendelezo wa Quds.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinai za kila aina zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni licha ya kuonekana kuchoka na kuongeza kuwa: Wanaodai kutetea haki za binadamu wa Ulaya na Marekani ambao walizusha makelele mengi kuhusiana na kadhia ya Ukraine, wamenyamaza kimya mbele ya jinai zinazofanyika huko Palestina na wala hawawatetei watu wanaodhulumiwa, bali kinyume chake wanamsaidia mbwa mwitu mwenye kiu ya damu. 

Siku ya Kimataifa ya Quds iliyotangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu, zaidi ya miaka 40 iliyopita huadhimishwa katika Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa maandamano, matamasha, semina na mikutano ya kutangaza uungaji mkono wa Umma wa Kiislamu na wapigania haki na uhuru kote duniani kwa Wapalestina wanaoendelea kuuawa na kukandamiza na utawala haramu wa Israel.

4053637

captcha