IQNA

Msikiti wa Al Aqsa wahujumiwa

Iran yalaani vikali kitendo cha Wazayuni kuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa

16:54 - May 30, 2022
Habari ID: 3475313
TEHRAN (IQNA)- Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhurii ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali hatua ya Wazayuni ya kuuvunjia heshima msikiti mtakatifu wa al-Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu. Msikiti huo uko katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Saeed Khatibzadeh, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  amesisitiza kuwa,  Quds au Beitul-Muqaddas ni mji mkuu wa daima wa taifa la Palestina.

Khatibzadeh sambamba na kupongeza hatua ya kusimama kidete wananchi wa Palestina na walinzi wa Quds mbele ya hatua za kichokozi na kichochezi za Wazayuni amekumbusha kwamba, malengo ya Quds ni katika mambo yanayopewa kipaumbele na ulimwengu wa Kiislamu.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhurii ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, ni jukumu la watu wote huru ulimwenguni hususan wananchi wa mataifa ya Kiislamu kuuhami kwa pande zote mji wa Qudss na kukabiliana na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Jumapili ya jana zaidi ya walowezi 1,000 wakisaidiwa na kupatiwa himaya na wanajeshi wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel waliingia katika eneo la ndani la Msikiti wa al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi sambamba na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Maandamano ya Bendera ya walowezi wa Kizayuni yameendelea kulaaniwa katika kila kona ya ulimwengu wa Kiislamu. Ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imelaani vikali maandamano hayo ya kichochezi na kubainisha kwamba, utawala ghasibu wa Israel unacheza na moto.

4060608

captcha