IQNA

Kadhia ya Palestina

UN yasisitiza lazima Israel iache kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina

12:29 - June 09, 2022
Habari ID: 3475354
TEHRAN (IQNA)- Timu ya ngazi ya juu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa imesema hatua ya utawala haramu wa Israel ya kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuwafanyia Wapalestina vitendo vya kibaguzi ndio sababu kuu ya kushuhudiwa mawimbi ya ghasia zisizokwisha katika ardhi hizo zilizoghusubiwa.

Katika ripoti yake ya kurasa 18 iliyotolewa  Jumanne, jopo hilo lililoteuliwa mwaka jana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeulaumu utawala wa Tel Aviv kwa mgogoro unaoshuhudiwa kwa miongo kadhaa sasa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, kutokomeza ukaliaji wa mabavu wa Israel, kunasalia kuwa nukta muhimu ya kumaliza msururu wa migogoro na ghasia hizo zisizokwisha.

Hata hivyo timu hiyo ya UN imeeleza bayana kuwa, Israel haina azma ya kuacha tabia yake hiyo ya kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Navi Pillay, Mtafiti mkuu wa timu hiyo ya Umoja wa Mataifa ambaye amewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN amesema, matokeo na mapendekezo ya tafiti za huko nyuma yameonesha kuwa, mzizi na chimbuko la migogoro katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni Israel.

Israel ilikataa katakata kushirikiana na Kamisheni ya Uchunguzi iliyoundwa mwaka jana na UN, kufuatia vita vya siku 11 katika Ukanda wa Gaza, ambavyo vinajulikana kama "Vita vya Upanga wa Quds."

Wapalestina 260 wakiwemo watoto wadogo 60 waliuawa shahidi kwa kudondoshewa mabomu na utawala pandikizi wa Israel katika Gaza, kuanzia Mei 10 mwaka jana na kuendelea kwa siku 11.

3479230

captcha