IQNA

Uislamu na Ukriso

Papa Francis apokea ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

16:25 - June 01, 2022
Habari ID: 3475324
TEHRAN (IQNA)- Mkurugenzi wa Vyuo vya Kiislamu nchini Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani na kumkabidhi ujumbe wa maneno kutoka kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Ayatullah Alireza Arafi Mkurugenzi wa Vyuo vya Kiislamu (seminari za Kiislamu) nchini Iran katika mkutano huo uliofayika Jumanne Vatican amesema: "Baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kupata taarifa kuhusu safari yangu amenitaka nikufikishie salamu zake. Aidha amepongeza  historia yako na uhusiano wako na Amerika ya Latini. Pia amepongeza baadhi ya misimamo yako kuhusu kuboresha uhusiano wa Uislamu na Ukristo na kutetea wanaodhulumiwa. Amesisitiza kuwa, sisi tunataraji kuwa utachukua misimamo ya wazi katika kuwatetea waliodhulumiwa kote ulimwenguni hasa mataifa ya Palestina na Yemen."

Ayatullah Arafi ameongeza kuwa: "Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anataraji kuwa, hatua zitachukuliwa kuwatetea watu wa Palestina na utatuzi wa kadhia ya taifa lao kwa msingi wa kura za wananchi na uchaguzi utakaowashirikisa watu asili wa Palestina ambao ni wafuasi wa dini zote ili mfumo wa utawala uundwe Palestina."

Papa Francis kwa upande wake amesema: "Mfikishie salamu zangu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Marajii wakubwa wa kidini Iran. Sisi pia tunakubali masuala ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema."

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Papa Francis ni mzaliwa wa Argentina na kwa muda mrefu alikuwa Askofu Mkuu wa mji mkuu, Buenos Aires.

Ayatullah Arafi anatembelea Vatican na Italia kwa mwaliko rasmi wa vituo vya kielimu na viongozi wa kidini.

Mapema katika barua mbili tofauti, maulama mashuhuri wa Kishia Ayatullah Makarem Shirazi na Ayatullah Jafar Sobhani walikuwa wamekaribisha safari hiyo, wakimtaka Ayatullah Arafi kutafuta njia za kupanua ushirikiano na Vatican katika nyanja mbalimbali zenye maslahi kwa pande zote. 

4061218  

captcha