IQNA

18:42 - March 06, 2021
News ID: 3473707
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Kiislamu nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani amekutana na Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ambapo katika mji mtakatifu wa Najaf, Iraq.

Kwa mujibu wa taarifa katika mkutano huo wa leo Jumamosi, viongozi hao wamejadili kadhia ya Palestina na umuhimu wa wafuasi wa dini mbali mbali kuishi kwa maelewano.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Ayatullah Sistani imesema katika mkutano huo wa kihistoria, wawili hao walizungumza kuhusu changamoto zinazoikabili jamii ya mwanadamu leo na nafasi ya Imani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na masuala ya maadili na changamoto zilizopo kuhusiana na maudhui hizo.

Katika kikao hicho, Ayatullah Sistani aliashiria matatizo na masaibu yaliyopo katika nchi za Asia Magharibi kama vile vita, vikwazo vya kiuchumi, watu kufurushwa makwao na hasa yanayojiri Palestina.

Taarifa hiyo imesema Ayatullah Sistani alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kidini katika kutatua matatizo yaliyopo. Aidha imearifiwa kuwa Ayatullah Sistani alisisitiza kuhusu jitihada za kustawisha thamani kama vile watu kuishi pamoja kwa amani na pia wafuasi wa dini mbali mbali kuheshimiana.

Mwanazuoni na kiongozi huyo wa ngazi za juu wa Kiislamu nchini Iraq aidha amesisitiza kuhusu raia Wakristo nchini Iraq kuishi kwa amani kama Wairaqi wengine na haki zao za kikatiba ziheshimiwe.

Nayo taarifa ya Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, imesema mkutano huo ulidumu kwa muda wa dakika 45 ambapo Papa Francis alimshukuru Ayatullah Sistani na Jamii ya Mashia kwa uungaji mkono wao kwa wanaodhulumiwa na pia kwa kutetea umoja wa Iraq.

Papa Francis pia amesisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano,urafiki na mazungumzo baina ya wafuasi wa dini mbali mbali.

Papa Francis aliwasili Baghdad Ijumaa ya jana tarehe 5 Machi na kulakiwa na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi. Katika safari hiyo ya siku tatu kiongozi wa Kanisa Katoliki atakutana na Wakristo wa Iraq, viongozi wa kidini na maafisa wa serikali ya nchi hiyo. Kabla ya safari hiyo Papa Francis alisema anataka kukutana na watu waliokumbana na mashaka mengi katika miaka ya hivi karibuni. 

3957809

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: