IQNA

Ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu

12:24 - June 09, 2022
Habari ID: 3475353
TEHRAN (IQNA)- Utafiti mpya umefichua kuwa, Waislamu saba kati ya kumi nchini Uingereza wamekabiliwa na vitendo vya chuki na ubaguzi kwa misingi ya dini yao.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la Savanta ComRes, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu barani Ulaya na hususan nchini Uingereza vimeongezeka kwa kiwango cha kutisha.

Utafiti huo umeeleza kuwa, asilimia 69 ya Waislamu walioajiriwa nchini UK, wamewahi kukumbwa na vitendo vya ubaguzi na udhalilishaji dhidi yao wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

Matokeo ya utafiti huo uliofanywa baina ya Aprili 22 na Mei 10 mwaka huu yameweka bayana kuwa, asilimia 42 ya Waislamu wa Uingereza wamekumbana na vitendo vya 'Islamophobia' katika mtagusano wao na wateja, wanunuzi na wafanyakazi wenzao. 

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na shirika la Savanta ComRes, asilimia 42 ya Waislamu katika nchi hiyo ya Ulaya wamefanyiwa vitendo vya chuki kwa kuwa ni Waislamu katika hafla za kijamii zinazohusiana na kazi, huku wengine asilimia 40 wakikabiliwa na vitendo hivyo walipotaka kupandishwa vyeo kazini.

Katika hali ambayo vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu vilivyoripotiwa nchini Uingereza kwa mujibu wa utafiti huo ni kwa kiwango cha asilimia 32, lakini hujuma hizo za kibaguzi dhidi ya Waislamu weusi nchini humo ni asilimia 58.

Hivi karibuni, Mbunge mwanamke wa Kiislamu katika Bunge la Uingereza, Zarah Sultana alisema: Nilidhani kwamba hali ya hujuma na chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza itaboreka lakini ukweli ni kinyume chake, kwa sababu Islamophobia na chuki dhidi ya Waislamu hapa nchini ni hakika ambayo haiwezekani kuificha.

3479223

captcha