IQNA

Polisi wa Uingereza Wachunguza Tukio la Matusi ya Maneno Nje ya Msikiti wa Suffolk

21:25 - July 12, 2025
Habari ID: 3480931
IQNA – Polisi nchini Uingereza wameanzisha uchunguzi kupitia kamera za usalama (CCTV) kufuatia tukio lililoripotiwa la matusi ya maneno dhidi ya waumini nje ya msikiti ulioko Haverhill, Suffolk.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi wa Suffolk, tukio hilo lilitokea mnamo saa 1:15 jioni siku ya Jumatatu, tarehe 7 Julai, wakati mwanamume mmoja aliyekuwa akiendesha baiskeli alikaribia msikiti uliopo barabara ya Campus. Inaripotiwa kuwa alitoa lugha ya matusi kwa watu waliokuwa eneo hilo.

Gazeti la East Anglian Daily Times limeripoti kuwa tukio hilo linachukuliwa kama kosa la kuvuruga amani lililoambatana na chuki za kidini au za kikabila.

Mtuhumiwa huyo ameelezwa kuwa alivaa fulana ya buluu yenye kamba nyeupe. Pia alivalia kaptula nyeusi na kofia ya michezo ya rangi nyeusi.

Mwanamume huyo alikuwa akiendesha baiskeli yenye rangi nyeupe na nyeusi, na alionekana akipita kati ya maeneo ya Burton End na Camps Road karibu na muda wa tukio.

Polisi wanatoa wito kwa yeyote anayemfahamu mtu huyo au mwenye taarifa muhimu kuwasiliana nao. 

3493799

captcha