Ameyasema hayo katika kipindi cha runinga cha asubuhi cha ITV "This Morning," Cooper ambapo amekiri kuwa awali serikali ya chama cha Labour ilikataa kukukubali kuwa wazungu wenye misimamo mikali ndio walioibua vurugu hizo zilizozuka Jumanne kufuatia tukio la kuchomwa kisu na kusababisha vifo vya watoto watatu.
Taasisi ya Tell Mama inayofuatilia hisia za chuki dhidi ya Uislamu nchini Uingereza kwa mara nyingine tena imehtahadharisha kuhusu vitendo vya kuibua na kutia hofu vinavyofanywa na watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia dhidi ya Waislamu nchini humo.
Vitendo vya Uasi na ghasia za makundi ya kibaguzi na yanayopinga wahajiri na Waislamu vimeongezeka katika wiki ya karibuni katika miji kadhaa ya Uingereza. Mashambulizi dhidi ya misikiti, maeneo ya ibada ya Waislamu, makazi ya raia, vituo vya biashara, kuibiwa maduka yao na pia mapigano na polisi hadi sasa vimesababisha kujeruhiwa makumi ya watu wakiwemo polisi. Hali hii ya mambo imetajwa kuwa changamoto kwa serikali mpya ya Uingereza.
Taasisi ya Tell Mama imetangaza kuwa, wiki moja iliyopita watu na makundi ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Uingereza waliwashambulia Waislamu na mbali kushambulia misikiti walitishia kuwaua na kuwabaka Waislamu.
Ripoti ya Taasisi ya Tell Mama imebainisha kuwa, vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu nchini Uingereza vimeongezeka mara tatu huku misikiti 10, ikiwa ni pamoja na huko Southport, Hartlepool na Liverpool ikishambuliwa na kupewa vitisho na watu wenye itikadi kali wa mrengo wa kulia na kupelekea idadi kubwa ya Waislamu kutoroka majumbani kwao hasa wanawake wanaovaa vazi la hijabu wakihofia kushambuliwa mitaani.
Gazeti la The Independent linalochapishwa nchini Uingereza limeripoti kuwa ghasia katika miji kama vile Liverpool, Leeds na Belfast ziligeuka kuwa machafuko makubwa mwishoni mwa juma, wakati watu wenye siasa kali za mrengo wa kulia walipopigana na polisi wa kutuliza ghasia, huku kukiripotiwa matukio mengi ya mashambulizi dhidi ya jamii za waliowachache hususan Waislamu katika mitaa ya miji kadhaa ya nchi hiyo.
Katika ripoti mbili tofauti, gazeti hilo limeeleza mlolongo wa ghasia zilizoikumba Uingereza kuwa ni hujuma za kibaguzi. Limeongeza kuwa, madai ya uongo yaliyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii yamechochea hisia za chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi, kwa kudai kuwa mshukiwa wa mauaji ya wasichana watatu katika jiji la Southport (kaskazini-magharibi mwa Uingereza) alikuwa Mwislamu anayetafuta hifadhi na kwamba aliwasili nchini humo kwa boti.
3489395