Ripoti hiyo, iliyochapishwa na kituo cha tafiti cha Equi, imesambazwa miongoni mwa Waislamu wa Uingereza sambamba na sherehe za Idd al-Adha. Inasisitiza kuwa kuna ongezeko la matamshi ya chuki na vitendo vya ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu, japokuwa tafiti zilizofanywa na Savanta/ComRes zinaonyesha kuwa wengi wa Waingereza wana mtazamo wa kutoegemea upande wowote au wa huruma kuhusu Waislamu.
Equi imeeleza kuwa mtazamo huu chanya wa wengi ni fursa ya mabadiliko ya kuboresha hali ya mambo. Ripoti inasisitiza umuhimu wa kujenga imani, ujumuishaji wa kila jamii, na uimara wa kiraia kama vipaumbele vya dharura vya kitaifa.
Profesa Javed Khan, mkurugenzi mkuu wa Equi, alisema: "Utambulisho wa kitamaduni uliojaa mchanganyiko na ukarimu wa Uingereza ni moja ya nguzo zake kuu. Lakini hatuwezi kuacha mshikamano wa kijamii kuwa jambo la bahati nasibu." Aliongeza kuwa kupuuza mgawanyiko wa kijamii siyo tu ni dhulma, bali pia ni mzigo mkubwa kifedha, hasa nyakati hizi za uhaba wa rasilimali.
Ripoti hiyo inatambua chuki dhidi ya Uislamu kama kikwazo kikubwa katika kujenga imani miongoni mwa jamii, hasa kufuatia machafuko ya kiangazi ya mwaka 2024. Makadirio yanaonyesha gharama za kiuchumi za chuki hiyo mwaka 2023 zilifikia pauni milioni 243 (takribani dola milioni 329), ikiwa ni pamoja na gharama za ulinzi, sheria, magereza, na bima.
Vilevile, ripoti hiyo ilikosoa baadhi ya sera za serikali kama vile mkakati wa "Prevent", na ikabainisha nafasi ya upotoshaji wa habari katika kudhoofisha mtazamo wananchi kuhusu Uislamu. Waislamu wengi nchini Uingereza wanahisi kuwa wanalengwa kupita kiasi na kutengwa na jamii nzima.
Miongoni mwa mapendekezo ya msingi ya ripoti hiyo ni kampeni za elimu ya umma kupinga mitazamo potofu, na mpango wa serikali kushirikiana na serikali za mitaa, taasisi za dini, na asasi za kiraia ili kurejesha imani. Pia inapendekeza kuwekeza zaidi katika vijana na programu za kijamii kwa lengo la kukuza ushiriki jumuishi na ujenzi wa uzoefu wa pamoja.
Equi ilieleza kuwa takwimu za maoni ya umma zinazodhihirisha moyo wa uwazi ni msingi mzuri wa kutengeneza sera. Profesa Khan alihitimisha kwa kusema: "Kutambua kwamba Waingereza wengi hawajavutwa na lugha za chuki zinazoweza kuharibu mahusiano ya kijamii kunapaswa kutupa matumaini makubwa. Serikali inapaswa kutumia nafasi yake ya kipekee kuwasilisha maono ya umoja wa kitaifa—wa maadili ya heshima, usawa na uhuru."
3493398