
Taasisi hiyo imeeleza katika taarifa kwamba, ilithibitisha kesi 5,837 za chuki dhidi ya Waislamu- ukiwa ni mchanganyiko wa matukio ya mitandaoni na yaliyolenga watu moja kwa moja - mwaka jana, ikilinganishwa na kesi 3,767 za mwaka wa kabla yake wa 2023 na 2,201 katika mwaka 2022.
Ukusanyaji wa taarifa unaofanywa na Tell MAMA ulianza mwaka 2012 na unafanyika kwa makubaliano ya kupatiana taarifa na vikosi vya polisi vya Uingereza na Wales.
"Mzozo wa Mashariki ya Kati ulichochea kupita kiasi chuki za mitandaoni dhidi ya Waislamu," imeeleza asasi hiyo katika taarifa yake hiyo, na kuongeza kuwa "vita vya Israel dhidi ya Ghaza, mauaji na machafuko ya Southport... vilisababisha kuongezeka visa vya chuki dhidi ya Uislamu vilivyoripotiwa kwa Tell MAMA kuanzia 2023-2024".
Mkurugenzi wa Tell MAMA, Iman Atta, amesema, ongezeko hilo ni jambo lisilokubalika na linatia wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali itakavyokuwa katika siku za usoni.
Tell MAMA, ambayo maana yake Upimaji wa Mashambulio Dhidi ya Waislamu (Measuring Anti-Muslim Attacks) inajitambulisha kama asasi huru, isiyo ya kiserikali inayofanya kazi ya kukabiliana na chuki dhidi ya Waislamu.
Kwa mujibu wa tasisi hiyo, kuongezeka kwa matukio ya chuki dhidi ya Waislamu yanayotokana na uenezaji chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) kumehusishwa pia na mauaji ya wasichana watatu katika mji wa kaskazini mwa Uingereza wa Southport yaliyotokea wakati wa msimu wa joto uliopita, wakati taarifa za uwongo ziliposambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba aliyehusika na mauaji hayo, -ambaye tangu wakati huo anatumikia kifungo cha miaka 52 jela-, alikuwa mhamiaji Muislamu mwenye itikadi kali, na hivyo kusababisha machafuko ya kibaguzi yaliyohusisha vikundi vya siasa kali za mrengo wa kulia na vile vinavyopinga uhamiaji nchini Uingereza.
3491918