Megan Rimmer, 36, ambaye alishuhudia shambulio hilo, alielezea tukio hilo la kuogofya: "Wote wawili walikuwa wakipitia lango moja na yule mzungu aligeuka tu na kumrukia kwa kisu.”
Rimmer, ambaye alikuwa na binti zake wakati huo, alimuona mtu huyo anayeaminika kuwa Mwislamu, akiwa amesimama huku damu ikimwagika kutoka mkononi mwake.
Baada ya kuhakikisha usalama wa watoto wake, alimsaidia mwanamume huyo aliyejeruhiwa kwa kufunga mkono wake na Keffiyeh aliyekuwa amevaa. Keffiyeh ni kitambaa ambacho huvaliwa kichwani na Waislamu wengu hasa wa Mashariki ya Kati.
Waislamu kote nchini Uingereza wamebainisha hofu hofu kuhusu usalama wao huku kukiwa na mashambulizi ya chuki dhidi ya Uislamu na ghasia za mrengo wa kulia kufuatia shambulio la visu huko Southport ambalo lilipelekea kuuawa wasichana watatu.
Vikundi vya jamii za Kiislamu vimewataka polisi kuimarisha ulinzi na doria nje ya misikiti kwani magenge ya wazungu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia wamepanga angalau mikutano 19 kote Uingereza katika siku zijazo.
Gazeti la The Times la Uingereza limeripoti kwamba madai ya uongo kwenye tovuti ya habari ya kutatanisha yamezua wimbi la hasira katika jiji la Southport (kaskazini-magharibi mwa Uingereza), kwa msingi wa tukio la mauaji ya wasichana watatu wadogo lililotokea katika mji huo mapema Jumatatu iliyopita.
Mji wa Southport, karibu na jiji la Liverpool, ulishuhudia makabiliano makali siku hiyo kati ya kundi la wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na polisi wa Uingereza nje ya Msikiti wa Southport Islamic Society. Msikiti huo ulizingirwa wakati ghasia zilipozuka Jumanne jioni, na zaidi ya maafisa 50 wa polisi walijeruhiwa huku washambuliaji wenye siasa kali za mrengo wa kulia wakitoa nara za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Gazeti la The Times limeripoti kwamba, tovuti ya "Channel 3 Now," ilichapisha habari feki na ya kupotosha mtandaoni ambayo ilimhusisha kwa uongo muomba ukimbizi bandia na tukio la kuchomwa visu watoto hao watatu.
Uongo huu ulienea haraka katika kipindi cha chini ya masaa 24 na kuwa vurugu na ghasia kubwa, ambazo gazeti hilo limeeleza kuwa ni moja ya kampeni zilisosambaa haraka sana za uongo nchini Uingereza katika enzi ya mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, televisheni ya BBC News wa Uingereza umeripoti kuwa mshukiwa wa mauaji hayo ni mzaliwa wa Cardiff kwa wazazi wenye asili ya Rwanda na alihamia eneo la Southport mwaka 2013 na wala si mhajiri Muislamu muomba hifadhi kama ilivyodaiwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Times, Channel 3 Now imeomba radhi na kufuta chapisho lililokuwa likirusha kwenye jukwaa la X (zamani Twitter), lakini jina la Muislamu ambaye ilidai kuwa ndiye mhusika wa uhalifu huo bado linaendelea kusambaa mtandaoni.
Baraza la Waislamu wa Uingereza (MCB) pia limetoa wito wa kuongezwa ulinzi. Zara Mohammed, katibu mkuu wa MCB, aliangazia wasiwasi ulioenea: "Kuna kiasi cha wasiwasi na hofu katika wikendi ijayo. Pia nina wasiwasi sana kutokana na matukio tuliyoyaona huko Southport na hata karibu na Downing Street ambayo yanawashirikisha majambazi na makundi ya watu wa mrengo wa kulia."
3489349