IQNA

Walowezi wa Kizayuni

Walowezi wa Israel wamuua mtoto wa Kipalestina karibu na Ramallah

19:49 - July 30, 2022
Habari ID: 3475558
TEHRAN (IQNA) – Mtoto wa Kipalestina alifariki dunia masaa mawili baada ya kupigwa risasi na walowezi wa utawala wa Kizayuni wa Israel waliokuwa na silaha siku ya Ijumaa karibu na kijiji cha Al-Mughayer, karibu na Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Amjad Nashaat Abu Alia, 16, alipigwa risasi wakati walowezi wa Kizayuni walipofyatua risasi za moto kwa washiriki katika maandamano ya kupinga shughuli za makazi haramu ya walowezi hao, amesema chifu wa baraza la kijiji Amin Abu Alia.

Amin alisema walowezi walifyatua risasi kwenye maandamano hayo wakiwa wanapata himaya ya wanajeshi wa Israel waliokuwepo.

Wizara ya Afya ya Palestina ilisema katika taarifa yake kwamba Amjad "alikufa kutokana na majeraha mabaya aliyopata kutokana na risasi za moto kifuani".

Watu wengine wanne walijeruhiwa kwa risasi za moto na zilizofunikwa kwa mpira, shirika la Al-Araby Al-Jadeed, liliripoti.

Mwanaharakati Kadhim Al-Hajj Mohammed alisema walowezi waliwashambulia waandamanaji wa Kipalestina chini ya ulinzi wa majeshi ya Israel.

Watu kadhaa walipata matatizo ya kupumua walipovuta gesi ya kutoa machozi, aliongeza, akisema waliojeruhiwa kwa moto walipelekwa katika hospitali ya Ramallah ya Istishari.

Jeshi la Israel lilidai kuwa liliingilia kati baada ya "mamia ya Wapalestina kuanzisha ghasia kali".

Mpiga picha wa AFP katika eneo la tukio aliripoti Wapalestina 300 hadi 400 walikusanyika kwa maandamano ya kupinga upanuzi wa makaazi ya Waisraeli katika eneo la Al-Mughayer.

Wapalestina wengine 11 walijeruhiwa wakati vikosi vya Israeli vilipokandamiza maandamano ya amani ya kila wiki katika kijiji cha Beit Dajan karibu na Nablus, kulingana na mwandishi wa habari Mohammed Abu Thabet.

Mmoja alijeruhiwa na risasi za mpira, huku wengine wakijeruhiwa kwa mabomu ya machozi wakati wa maandamano yaliyotoka msikitini katika kijiji hicho hadi makazi ya Waisraeli yaliyoko kaskazini-mashariki yake, Abu Thabet alisema.

Vikosi vya Israel viliyazima maandamano hayo yalipowasili kwenye makazi hayo, aliongeza, akisema wanajeshi walitumia kioo kuwazuia waandishi wa habari kufanya kazi yao.

Pia walikandamiza maandamano mengine ya kupinga kituo cha makazi cha Evyatar kilichoko kwenye Mlima Sabih, pia karibu na Nablus, mwandishi wa ndani Majdi Hamayel alisema.

Mkurugenzi wa idara ya dharura wa Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina Nablus, Ahmad Jibril, alisema kuwa katika eneo la Mlima Sabih wafanyakazi wa gari la wagonjwa walimtibu mtu mmoja aliyejeruhiwa kwa risasi za mpira, wengine watano kujeruhiwa kwa mabomu ya machozi, na mwingine aliyejeruhiwa baada ya kuanguka.

Kwa muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni umekuwa ukiteka ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa lengo la kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii katika maeneo ya Wapalestina kwa uungaji mkono wa kila upande wa Marekani.

Utawala wa Kizayuni unaendeleza ujenzi huo haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina huku ukipuuza takwa la jamii ya kimataifa la kusimamisha ujenzi huo kwa kukingiwa kifua na Marekani. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ujenzi wa vitongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ni kinyume cha sheria.  

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hadi sasa utawala wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. 

3479893

Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha