IQNA

Kombe la Dunia la Qatar

Mufti wa Oman awashukuru Waislamu kwa kuwasusia waandishi habari Wazayuni

14:02 - November 28, 2022
Habari ID: 3476163
TEHRAN (IQNA) - Mufti mkuu wa Oman amewashukuru Waislamu na wale wote ambao wamekataa kuzungumza au kuhojiwa na na waandishi wa habari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati wa Kombe la Dunia la 2022 linaloendelea nchini Qatar.

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya Twitter, Mufti Mkuu wa Oman Sheikh Ahmed Bin Hamad Al-Khalili ametoa shukrani kwa wale ambao wamewapuuza Wazayuni.

Amewapongeza Waqatari, Waarabu na Waislamu  waliokataa kuzungumza na waandishi habari utawala haramu wa Israel na kuwataja Wazayuni kuwa ni wavamizi ambao hawana haki katika ardhi za Palestina.

Amesema kukataa huko kunaonyesha hali nzuri ya mwamko katika Umma wa Kiislamu.

Matamshi hayo yanakuja huku kumekuwa na ripoti nyingi za kukataliwa kwa waandishi wa habari wa Israel wakati wa hafla hiyo na mashabiki wa Kiarabu.

Ripota wa Idhaa ya 12 ya Israel alikiri kwamba "karibu mashabiki wote wa Kiarabu tunaokutana nao na kujitambulisha kwa ujumla hukataa kuzungumza nasi. Kulikuwa na kundi la vijana wa Lebanon, ambao mtazamo wao ulibadilika digrii 180 wakati tulipowaambia kwamba sisi tunatoka Israeli."

Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha mashabiki wa Lebanon wakiondoka mara tu mwandishi aliposema, "Mimi natoka Israel," wakimuuliza "mbona hata uko hapa?" "Hakuna kitu kama Israeli. Ni Palestina. Israel haipo," alisema shabiki huyo wa Lebanon.

Video nyingine ilionyesha mashabiki wawili wa Saudia wakikataa kuzungumza na mwandishi baada ya kusema kuwa anatoka "TV ya Israel."

Watumiaji wa mitandao ya kijamii hapo awali walikuwa wamechapisha video fupi inayoonyesha raia wa Qatar akikataa kuhojiwa na idhaa ya Israel huko Souq Waqif mjini Doha.

Moja ya matukio ya kuvutia katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar ni kukataa wananchi wa mataifa mbalimbali ya Kiarabu kuhojiwa na vyombo vya habari vya Israel na vilevile kuiunga mkono Palestina dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.

Kimsingi, Kombe la Dunia ni uwanja wa kujionea mandhari za maamiliano baina ya watu; mandhari ambazo ni nadra kushuhudiwa katika siku zingine kwenye nchi mbalimbali duniani. Halikadhalika, Kombe la Dunia ni jukwaa la watu kutoka nchi mbalimbali kufahamiana, na pia ni ulingo wa makabiliano ya kijamii na kimichezo baina ya nchi maalumu.

Harakati hiyo ya watazamaji kutoka mataifa ya Kiarabu katika Kombe la Dunia la Qatar inaakisi nukta muhimu kadhaa za kijamii na kisiasa.

Nukta ya kwanza ni kwamba; katika nchi za Kiarabu, licha ya utegemezi walionao baadhi ya watawala wa nchi hizo kwa Magharibi na kuwa kwao kitu kimoja na utawala wa Kizayuni, wananchi Waislamu wa mataifa hayo wanapinga vikali hatua ya kuanzisha uhusiano na Israel; na badala yake wanaunga mkono piganio tukufu la ukombozi wa Palestina.

Nukta ya pili ni kuwa; harakati ya watazamaji wa mataifa ya Kiarabu kwa vyombo vya habari vya Israel na waandishi wake wa habari inaashiria mpasuko uliopo kati ya wananchi hao na baadhi ya tawala za Kiarabu juu ya suala la Palestina. Wakati serikali za Kiarabu zimeliweka pembeni suala la Palestina na kushupalia kuanzisha uhusiano na utawala unaokalia Quds tukufu kwa mabavu, kwa wananachi wa mataifa ya Kiarabu, suala la Palestina lingali ndilo suala kuu na la kiutambulisho kwao. Kwa hivyo, Kombe la Dunia nchini Qatar limedhihirisha upana mkubwa wa mapasuko uliopo kati ya matakwa ya wananchi na sera zinazofuatwa na tawala za Kiarabu.

Na nukya tatu ni kwamba; harakati iliyoonyeshwa na watazamaji kutoka mataifa ya Kiarabu dhidi ya waandishi wa habari na vyombo vya habari vya Kizayuni inamaanisha kushindwa na kugonga ukuta pia mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Wakati watawala wa baadhi ya nchi za Kiarabu wanazuia kufanyika maandamano yoyote ya kupinga mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ndani ya nchi zao, Kombe la Dunia la Qatar limegeuzwa kuwa fursa kwa wananchi wa nchi mbalimbali za Kiarabu kubainisha upinzani wao dhidi ya mchakato huo. Hii inaonyesha kuwa kiuhalisia, mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ni mchakato uliofeli na kugonga mwamba, kwa sababu haujapata uungaji mkono wowote wa wananchi.

4102876

Kishikizo: Kombe la Dunia ، qatar ، ، wazayuni ، mufti wa oman
Jina:
Baruapepe:
* maoni:
captcha