IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Waislamu walaani kitendo cha maafisa wa BJP India kumvunjia heshima Mtume SAW

12:18 - June 06, 2022
Habari ID: 3475342
TEHRAN (IQNA)- Nchi za Kiislamu duniani zimeendelea kulalamikia vikali matamshi dhidi ya Mtume Mutukufu wa Uislamu, Muhammad SAW ambayo yalitolewa katika mdahalo wa Televisheni huko India na kuibua hasira miongoni mwa Waislamu duniani.

Katika mdahalo wa televisheni, msemaji wa chama tawala cha India, BJP, Nupur Sharma alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Mtume wa Uislamu, ambayo yamelaaniwa kote India na kuibua ghasia nchini humo. Jana Jumapili chama cha BJP kilitangaza kusimamisha uanachama wa Sharma na kujiweka mbali na matamshi yake yenye chuki.

Aidha chama hicho kimemfukuza Naveen Kumar Jindal ambaye anasismamia kitengo cha habari cha chama hicho mjini New Delhi ambaye pia alituma ujumbe uliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katika ukurasa wake wa Twitter na kufuatia malalamiko alifuta ujumbe huo.

Pakistan yataka jamii ya kimataifa iingilie kati

Baada ya kauli hizo zenye chuki dhidi ya Mtume Muhammad SAW, Pakistan imetoa taarifa na kulaani vikali kabisa kauli hizo na imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kuhusu hali mbaya ya chuki dhidi ya Uislamu nchini India.

Kuwait yataka wahusika waadhibiwe

Serikali ya Kuwait nayo imemuita balozi wa India na kumkabidhi malalmiko kufutia hali hizo zilizo dhidi ya Uislamu. Kuwait imesema inapinga vikali matamshi ya maafisa hao wa BJP na imetaka hatua dhidi ya wahusika zichukuliwe.

Qatar yataka India iombe msamaha rasmi

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imekaribisha hatua ya chama cha BJP kumsimamisha kazi afisa husika na kusema inataraji serikali ya India itatoa taarifa kwa umma kuomba radhi na kulaani matamshi hayo. Balozi wa India mjini Doha, Deepka Mittal ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar na kukabidhiwa malalamiko ya serikali ya Qatar.  Wakuu wa Qatar wanasema kuruhusu matamshi kama hayo yenye chuki dhidi ya Uislamu kupita bila adhabu ni ukiukaji wa haki za binadamu na jambo hilo litaibua ghasia na uhasama.

Iran yawasilisha malalamiko rasmi kwa India

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa India mjini Tehran kulalamikia vikali matamshi dhidi ya Mtume Mutukufu wa Uislamu, Muhammad SAW ambayo yalitolewa katika mdahalo wa televisheni nchini India.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Asia Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumapili alimuita Balozi wa India ili kubainisha malalmiko makali ya serikali na watu wa Iran kuhusu matamshi yaliyomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

Kwa upande wake, Balozi wa India alibainisha masikitikio yake kuhusiana na kadhia hiyo huku akisisitiza kuwa, kitendo chochote kile cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW hakikubaliki.

OIC yatahadahrisha kuhusu chuki dhidi ya Uislamu India

Kwa upande wake Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu  (OIC) imetoa taarifa na kulaani vikali matamshi hayo ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW na kusema yamekuja huku kukishudiwa kuongezeka chuki na uhasama dhidi ya Uislamu nchini India na ukandamizaji Waislamu nchini humo.

Ansarullah yasema ni uporomokaji maadili

Nayo harakati ya Ansarullah ya Yemen, kupitia msemaji wake, Mohammad Abul Salam, imelaani vikali matamshi hayo ya msemaji wa BJP dhidi ya Mtume Mtukufu wa Uislamu na kusema yanaashiria upromokaji wa maadili na ni jambo lisilokubalika.

Mufti wa Oman ataka Waislamu waamke

 

Kwa upande wake, Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed Al-Khalili, amelaani matamshi ya matusi yaliyotolewa na msemaji wa chama tawala cha India dhidi ya Mtukufu Mtume (SAW).

Kwa mujibu wa taarifa, Sheikh al-Khalili alitoa taarifa akikosoa matamshi hayo katika akaunti yake ya Twitter na kuyataja matamshi hayo ya matusi ya msemaji wa chama tawala cha India kuwa ni matusi kwa Waislamu wote.

Ameendelea kusema: "Uthubutu wa msemaji wa chama tawala cha itikadi kali cha India kutoa matamshi dhidi ya Mtume (SAW) ni vita dhidi ya Waislamu wote duniani." Mufti wa Oman ametoa wito kwa Waislamu duniani kuamka na kuwa na Umoja wa Kiislamu ili waweze kushughulikia vitendo viovu kama hivyo.

4062123

captcha