IQNA

Diplomasia

Rais Raisi: Afrika ni ardhi ya fursa ambayo haipasi kupuuzwa

21:07 - July 14, 2023
Habari ID: 3477279
TEHRAN (IQNA)- Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza haja ya kukuza uhusiano na mataifa ya Afrika, akilielezea bara hilo kama ardhi ya fursa na kwamba uwezo wake haupasi kupuuzwa.

Rais Raisi ameyasema hayo mapema leo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran akitokea kwenye ziara yake ya kuzitembelea nchi tatu za Kiafrika za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Amesema: "tunathamini uhusiano wetu na bara la Afrika, kama tunavyofanya na nchi za Asia na kanda zingine, na hatupaswi kulipuuza bara hili ambalo limejaa fursa".

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, baada ya kushuhudia imani ya kweli, moyo wa kupiga vita ukoloni na ujasiri wa watu wa Iran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, mataifa ya Afrika yamevutiwa na Mapinduzi hayo na mfumo uliotokana nayo.

Rais Raisi amebainisha kuwa lengo la kwanza la safari yake hiyo lilikuwa ni kuimarisha "kina cha stratejia" ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran barani humo.

Kuhusiana na lengo la pili la ziara yake ya kuzitembelea Kenya, Uganda na Zimbabwe, Seyed Ebrahim Raisi amesema ni kustawisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi za Afrika na kuingia katika masoko mapya kwa ajili ya bidhaa za kitaaluma zinazotengenezwa na wataalamu wa Iran.

Ameendelea kueleza kwamba, upatikanaji wa malighafi ni lengo jingine la ziara hiyo, akisema kuwa suala la kuanzisha ukulima wa nje ya nchi, nalo pia ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa.

Kwa mujibu wa Rais Raisi, makubaliano yamefikiwa kwa ajili ya mabadilishano ya kibiashara ya bidhaa ambapo Iran itapatiwa malighafi mkabala wa kuzipatia nchi za Afrika bidhaa za petrokemikali.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwa kusema: "kazi kubwa zaidi inapasa kufanywa kupanua uhusiano na mataifa ya Afrika katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kuliko ilivyokuwa wakati mwingine wowote,” na akaongeza kuwa kuboreshwa ushirikiano wa pande mbili na nchi hizo kutapelekea kuimarika ushirikiano katika uga wa kikanda na kimataifa.

Seyed Ebrahim Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa ulimwengu si nchi za Magharibi pekee, na akisisitiza kwamba sera ya kigeni ya Iran imejikita katika kujihusisha na dunia nzima. Ameongeza kuwa "Afrika ni muhimu kama ilivyo Amerika na Asia".

Jumla ya hati 21 za ushirikiano katika maeneo tofauti zilitiwa saini wakati wa ziara hiyo ya Rais Raisi ya kuyatembelea mataifa matatu ya bara la Afrika.

4154951

Kishikizo: Rais Raisi afrika uganda
captcha