IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jeshi la IRGC la Iran ni taasisi kubwa zaidi ya kupambana na ugaidi duniani

11:13 - August 18, 2023
Habari ID: 3477453
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran amesema kuwa, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ni taasisi kubwa zaidi ya kupambana na ugaidi duniani ambayo inafanya mambo makubwa ya kupigiwa mfano ambayo majeshi makubwa duniani yanashindwa kuyafanya.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo  Alkhamisi jijini Tehran wakati alipoonana na washiriki wa Kongamano la 24 Kuu la Makamanda na Maafisa wa Jeshi la IRGC au SEPAH na kuongeza kuwa, hakuna taasisi yoyote ya kijeshi ambayo imekamilika kiasi hiki katika upande wa usalama wa masuala ya kiroho na kimaanawi, kisiasa, kimaadili na kibinadamu kama lilivyo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Aliongeza kuwa, kuasisiwa, kukuwa, kustawi na kuwa imara katika kupambana na migogoro sambamba na kazi nyingine za Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC katika upande wa kijeshi, kutumikia wananchi, kutoa huduma na kazi za ujenzi wa taifa, kumelifanya jeshi hilo kuwa la kipekee na la kujivunia.

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, hakuna taasisi yoyote ya kijeshi ambayo imekamilika kiasi hiki katika upande wa usalama wa masuala ya kiroho na kimaanawi, kisiasa, kimaadili na kibinadamu kama lilivyo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu amegusia pia jinsi jeshi la IRGC linavyozidi kuimarika siku baada ya siku na kuongeza kuwa, hivi sasa jeshi hilo limekuwa ni kituo adhimu na kilichojizatiti kikamilifu kwa zana na silaha 

Vilevile amesema, kupungua na kutorudiwa kusemwa na maadui kwamba "chaguo la kijeshi dhidi ya Iran liko mezani," kunatokana na nguvu za kuzuia mashambulio za Jeshi la IRGC na kuongeza kuwa, watu wote wanatambua hivi sasa kwamba maneno hayo ya kuitishia kijeshi Iran yamepungua mno, hayana maana na yamepoteza mvuto.

Ayatullah Khamenei pia amesema, kazi za kujivunia na za mafanikio makubwa za jeshi la IRGC zimemlazimisha adui atafute njia nyingine za kukabiliana na jeshi hilo na sasa ameishia kueneza uongo, uvumi usio na msingi na upayukaji wa hapa na pale kwa shabaha ya kulichafulia jina jeshi hilo imara. 

Aidha amesema, moja ya sababu kuu za uadui inaofanyiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa kwake kigezo bora na kuwa kwake mstari wa mbele katika harakati za muqawama kwenye eneo nyeti la magharibi mwa Asia. Amesema, kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isingekuwa kigezo bora, uadui wote uliopo dhidi yake ungeondoka.

Amezungumzia pia jinsi majeshi makubwa ya nchi tatu za Kiarabu yalivyoshindwa kivita na utawala khabithi na afiriti wa Kizayuni katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran na kusisitiza kuwa, baada ya kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, hali imekuwa ngumu kwa utawala wa Kizayuni kiasi kwamba iliendesha vita kwa muda wa siku 33 vya kujaribu kuisambaratisha harakati ya Hizbullah lakini ilishindwa, bali ililazimika kukimbia kwa madhila huko kusini mwa Lebanon.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, hali hivi sasa imekuwa nzito kwa utawala wa Kizayuni kiasi kwamba, vijana wa maeneo ya Palestina yaliyoko magharibi mwa Mto Jordan yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni wanaendesha mapambano kwa namna ambayo wamelichosha jeshi la utawala wa Kizayuni ambalo wakati fulani lilikuwa linajigamba kuwa eti halishindiki.

Vilevile amesema, njama zote inazofanyiwa Iran zinapangwa na kuendeshwa na mashirika ya kijasusi ya Marekani CIA, lile la utawala wa Kizayuni la MOSSAD na MI6 la Uingereza.

Aidha amesema: Ni sawa kwamba viko vitimbakwiri vya ndani na nje na baadhi ya watu waliohadaiwa na Umagharibi, lakini kazi hasa inafanywa na mashirika hayo ya kijasusi.

4163096

captcha