IQNA

Kamanda wa Kikosi cha QUDS cha IRGC

Utawala wa Kizayuni uanze kutafakari kuondoka katika ardhi za Wapalestina

18:22 - May 30, 2021
Habari ID: 3473962
TEHRAN (IQNA) - Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema wakati umefika kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuanza kutafakari kuondoka katika ardhi za Palestina unaozikalia kwa mabavu haraka iwezekanavyo.

Brigedia Jenerali Ismail Qaani amesema hayo jana Jumamosi hapa mjini Tehran, katika kumbukumbu za kuadhimisha Arubaini ya Brigedia Jenerali Mohammad Hosseinzadeh Hijazi, aliyekuwa Naibu Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC ambaye aliaga dunia mwezi Aprili mwaka huu akiwa na umri wa miaka 65, kutokana na mshtuko wa moyo.

Brigedia Jenerali Qaani ameeleza bayana kuwa, Wazayuni wanapaswa kuondoka na kuzikabidhi ardhi walizozighusubu kwa Wapalestina, na warejee makwao huko Marekani na Ulaya. Amesema, "Nawashauri Waisraeli ambao waliuza majumba yao huko Marekani na Ulaya na kwenda Palestina, warejee walikotoka kabla ya bei za majumba hayo hazijaongezeka maradufu."

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la IRGC la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel hauwezi tena kulemaza mapambano ya Wapalestina kwa risasi na silaha, na kwamba kambi ya muqawama inazalisha silaha zote inazohitaji ndani ya maeneo yake ya kijiografia, yakiwemo makombora 3000 iliyoyavurumisha kuelekea Israel katika vita vya siku 12 vya hivi karibuni.

Hapo jana pia katika mahojiano na televisheni ya al-Masirah, Brigedia Jenerali Ismail Qaani alisema kuwa, bwabwaja na vitisho vya Wazayuni si kitu kingine bali upumbavu, kwa kuwa hivi karibuni tu Ukanda wa Gaza ambao uko chini ya mzingiro wa miaka mingi wa Israel ulitoa pigo kubwa kwa utawala huo pandikizi.

Ameongeza kuwa, " ni uongo kudai kuwa hakuna anayeweza kuushinda utawala wa Kizayun, hivyo vitisho vya shirika la kijasusi la utawala wa Kizayuni Mossad vya eti linaweza kuanzisha vita dhidi ya Iran, hususan baada ya kushindwa na muqawama wa Wapalestina, ni upuuzi tu."

Zama za kupiga na kukimbia zimekwisha

Kamanda Mkuu wa IRGC ameashiria kuongezeka nguvu ya Palestina na kusisitiza kuwa zama za piga na kukimbia zimekwisha.

Meja Jenerali Hussein Salami amesisitiza udharura wa kuzidishwa uwezo na nguvu ya Palestina na kueleza kuwa, Waisraeli wanapasa kuelewa kuwa zama zile za kupiga na kukimbia zimepita, na wananchi wa Palestina leo hii wana nguvu kubwa. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ameongeza kuwa Palestina mpya imedhihirika. Amesema kuwa, vita vya hivi karibuni vimeiingiza Palestina yenye nguvu katika mahesabu ya utawala wa Kizayuni.  

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amebainisha kuwa Wapalestina watazidi kupata nguvu siku baada ya siku. Meja Jenerali Hussein Salami amesisitiza pia kuwa, wananchi wa Iran wataitikia maelekezo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kushiriki kwa wingi katika uchaguzi.  

3974297

captcha