
Mazishi hayo yalihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi pamoja na viongozi wa Hizbullah. Akihutubia hafla hiyo, Sheikh Ali Damoush, Mkuu wa Baraza Kuu la Utendaji wa Hizbullah, alisema Shahidi Tabatabai hakuwa tu kamanda wa operesheni nyingi kwa kipindi cha miaka 35 iliyopita, bali pia alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa kupambana na uvamizi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon na mbunifu wa mikakati ya muqawama baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Sheikh Damoush aliongeza kuwa Tabatabai alikuwa mtu wa uwanja katika mapambano yote na mmoja wa waasisi wa uhuru na ushindi. Alibainisha pia kuwa Tabatabai ndiye aliyekuwa akiongoza mapambano yaliyofahamika kama “Awli al-Bas” na alihusika katika kuongoza muqawama, kupanga, kuandaa na kuchora mikakati ya mapambano baada ya kusitishwa kwa vita.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Damoush alisema kuwa ni wajibu wa serikali kulinda wananchi wake na uhuru wa taifa, na kusimama imara dhidi ya mashinikizo na maagizo ya kigeni. Alisisitiza: “Adui hajafahamu kuwa sisi katika Hizbullah tunakuwa imara na wakubwa zaidi kwa mashahidi, na Wazayuni wanapaswa kubaki na wasiwasi, kwa sababu wamefanya kosa kubwa.”
Sheikh Damoush alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mradi adui hatatii makubaliano ya kusitisha mapigano, “sisi hatulazimiki wala hatujifunge kwa mpango au pendekezo lolote.”
Usiku wa Jumapili, Hizbullah ilitangaza kuuawa kwa Kamanda Tabatabai pamoja na wapiganaji wengine wanne wa muqawama katika kile kilichoitwa “shambulio la hila la Israel.” Tabatabai ndiye kamanda mwandamizi zaidi wa Hizbullah kuuawa na Israel tangu makubaliano ya kusitisha mapigano ya Novemba 2024.
Taarifa ya IRGC
Wakati huo huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limesema kuwa mauaji ya kikatili yaliyofanywa na Israel dhidi ya kamanda wa ngazi za juu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon yamefichua “udhaifu” wa utawala huo mbele ya Mhimili wa Muqawama.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, IRGC imelaani vikali mauaji ya Haytham Ali Tabatabai katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, yaliyofanyika siku iliyotangulia.
Taarifa hiyo imesema:“Utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine tena umetenda kosa la wazi la kigaidi kwa kumlenga mmoja wa makamanda imara wa Hizbullah.”
“Kitendo hiki cha woga, kilichotokea wakati wa kile kinachodaiwa kuwa ni usitishaji vita ambao Waisraeli wamekuwa wakiuvunja mara kwa mara, si ishara ya nguvu bali kinaonesha udhaifu na kutokuwa na uwezo adui mbele ya azma ya mataifa ya eneo hili pamoja na Mhimili wa Muqwama.”
IRGC pia imebaini masikitiko yake juu ya ukimya na kutochukua hatua kwa mashirika ya kimataifa na ya haki za binadamu kuhusu mauaji ya kimbari na hujuma zinazofanywa na Israel, pamoja na uungwaji mkono ambao utawala huo unapata kutoka kwa watawala wa Marekani wanaochochea vita na kuendeleza ugaidi.
Aidha IRGC imesisitiza kuwa Mhimili wa Muqawama bado “uko hai na una nguvu” na kwamba damu ya mashahidi itawasha moto wa matumaini na msimamo imara katika nyoyo za wanaotafuta uhuru pamoja na wapiganaji waaminifu wa Muqawama kote eneo hili.
Halikadhalika IRGC imesema: “Bila shaka, Mhili wa Muqawama na Hizbullah ya Lebanon wana haki kamili ya kulipiza kisasi kwa damu ya wapiganaji hodari wa Uislamu. Muda utakapowadia, jibu kali na la kuumiza litatolewa dhidi ya mvamizi huyo wa kigaidi."
Katika taarifa hiyo hiyo, IRGC ilisema Umma wa Kiislamu unayaona mauaji hayo kama sehemu ya “vita vya kisaikolojia” vya Israel na “jaribio la mwisho la kukata tamaa” kuficha migogoro yake ya ndani pamoja na kushindwa kwake mara kwa mara katika medani ya vita. IRGC imeonya kwamba matendo kama hayo yataleta kushindwa kukubwa zaidi na kuongezeka kwa hasira na chuki ya dunia dhidi ya utawala huo ghasibu.
Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusema: "Mhimili wa Muqawama, kupitia juhudi za kijeshi, kisiasa, vyombo vya habari pamoja na uungwaji mkono wa wananchi, utaendelea kupambana hadi kupata ushindi wa mwisho dhidi ya wavamizi wa ardhi takatifu ya Palestina na Al-Quds (Jerusalem)."
3495517