IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Waislamu wakabiliane na Ujahiliya (Ujinga) unaoenezwa na Marekani

22:37 - May 05, 2016
Habari ID: 3470295
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, jukumu muhimu kabisa la Umma wa Kiislamu ni kukabiliana na harakati ya ujahiliya inayoongozwa na Marekani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo katika hadhara ya maafisa wa ngazi za juu wa Mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu hapa Tehran na kundi la  familia za Mashahidi kwa mnasaba wa maadhimisho ya Mab'ath na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW na kubainisha kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mstari wa mbele katika harakati ya kusukuma mbele gurudumu la Mab'ath iliayoanzishwa na Imam Ruhullah Khomeini MA, itaaendelea na njia yake hiyo bila ya kuogopa madola yenye nguvu duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Umma wa Kiislamu na taifa kubwa la Iran na kueleza kuwa, Siku kuu ya Maba'th ni Idi ya mwamko na harakati na siku ya kurejea katika fitra ya Mwenyezi Mungu na maisha yanayoambatana na utumiaji akili, uhuru, uadilifu na uja kwa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khaemenei amesema kuwa, jukumu la Mitume wa Mwenyezi Mungu lilikuwa ni kuwaongoza wanadamu kuelekea katika fitra na maumbile haya masafi katika kalibu ya maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu).

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, harakati ya Uzayuni inayotawala dunia ni mfano wa wazi wa uundaji mfumo wa mashetani na kwamba, hali ya leo ya dunia ni matokeo ya mtandao mpana wa mabepari wa Kizayuni.

Aidha Ayatullah Khamenei amesema, Marekani inachochea chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya Iran na chuki dhidi ya madhehebu ya Shia.Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuendelea kuwepo mapambano baina ya mrengo wa mab'ath na Utume na mrengo wa ujahilia tangu mwanzoni mwa kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu hadi leo hii na kusema kuwa, vielelezo vikuu vya mrengo wa mab'ath na Utume ni hekima na busara kubwa iliyoongozwa na Bwana Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na kielelezo kikuu cha mrengo wa ujahilia ni uasherati na ghadhabu na kuongeza kuwa: Jukumu kuu la umma wa Kiislamu leo hii ni kukabiliana na mrengo wa ujahilia unaoongozwa na Marekani na kwa upande wake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo iko mstari wa mbele katika mrengo wa kushikamana na mafundisho ya Mtume Muhammad SAW, itaendelea na njia yake iliyoanzishwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) ya kupambana na kukabiliana vilivyo na madola ya kibeberu bila ya woga wowote.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW kwa umma wa Kiislamu na kwa taifa kubwa la Iran na huku akitoa ushahidi kutoka katika aya za Qur'ani Tukufu amezungumzia maana pana na ya kina sana na kubaathiwa Bwana Mtume akisema: Siku ya kubaathiwa ni sikukuu adhimu na ni siku ya kurejea kwenye maumbile aliyoumbwa nayo mwanadamu na kuishi katika maisha ya hekima, mantiki, ukombozi, uadilifu na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kwamba kazi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu ni kuwaongoza wanadamu kuelekea kwenye maumbile hayo safi na kutakafari maumbile ya Mwenyezi Mungu na kutenda kila jambo kwa kuzingatia maamrisho ya Allah Mtukufu na kushikamana na tawhidi.
Vile vile ameashiria namna mwanadamu anavyohitajia muda wote mafundisho ya Mtume na kuutaja mrengo wa ujahilia kuwa ni kambi inayokinzana kikamilifu na mafundisho hayo ya Mtume. Ameongeza kuwa: Mrengo wa ujahilia hauhusiani tu na zama za Bwana Mtume Muhammad SAW, bali ni mrengo uliondelea kuwepo hadi leo hii ukikabiliana na mrengo wa kutafakari maumbile ya Mwenyezi Mungu unaoongozwa na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW ingawa leo hii mrengo huo wa ujahilia unatumia elimu na teknolojia ya zama hizi kuendeleza vita vyake kwa sura nyingine tofauti na ile ya zama za Bwana Mtume.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, uasherati, ghadhabu na hawaa za nafsi ndivyo vielelezo vikuu vya mrengo wa ujahilia na kuongeza kuwa: Matokeo ya vitendo vya kambi ya ujahilia siku zote ni mateso, matatizo, kumdhalilisha mwanadamu, kuua mamilioni ya watu, kupora mali za mataifa mengine na kueneza ufisadi duniani ambapo mfano wa wazi kabisa wa suala hilo ni vita viwili vikubwa vya kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia suala la kuzuka mirengo miwilli ya ujahilia na ule wa mafundisho ya Mtume Muhammad SAW katika upeo wa watu binafsi, wa kijamii na kimataifa na kuongeza kuwa: Kama katika upeo wa kimataifa mienendo ya madola yenye nguvu itaongozwa kwa busara za mafundisho ya Bwana Mtume SAW bila ya shaka yoyote dunia itakuwa kwa sura nyingine tofauti na itakavyokuwa wakati miamala na vitendo vya madola yenye nguvu vitakapoongozwa na hawaa za nafsi, kupenda ukubwa na kueneza fitna duniani.
Amesema, kukandamizwa mataifa ya dunia na madola ya kikoloni ni mfano mwingine wa wazi wa vitendo vya mrengo wa kijahilia na huku akiashiria madhara makubwa iliyopata India kutokana na ukoloni wa makumi ya miaka wa dola la kikoloni la Uingereza, amesema kuwa: Vita na fitna zilizoenea leo katika eneo la magharibi mwa Asia ni matokeo mengine ya vitendo vya kambi ya kijahilia na ya shetani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, mrengo wa Uzayuni unaotawala dunia hivi sasa ni mfano mwingine wa wazi wa mfumo wa mashetani na kusema: Hali ilivyo duniani leo ni matokeo ya kutawaliwa dunia na kanali pana ya mabepari wa Kizayuni ambao wamepenya na wana nguvu hadi ndani ya serikali kama ya Marekani na kwamba mrengo na chama chochote kile hakiwezi kupata nguvu na kuingia madarakani katika nchi hizo bila ya kuwa mfuasi wa mrengo huo wa Kizayuni.
Ayatulllah Udhma Khamenei ameutaja msingi mkuu wa harakati adhimu ya Umma wa Kiislamu na Iran pamoja na mwamko wa Kiislamu, kuwa ni kupambana na nguvu za mrengo huo fasidi wa Kizayuni na kuongeza kusema kwamba: Ni kwa sababu hiyo ndio maana leo hii siasa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu, dhidi ya Iran na dhidi ya Ushia zikawa ndizo sera kuu na zisizobadilika za Marekani na tawala zenye mfungano na dola hilo la kibeberu.
Vile vile ameutaja mwamko na kuwa macho taifa la Iran na mataifa ya Kiislamu katika kukabiliana na harakati za kiharibifu na kifisadi za madola ya kibeberu kuwa ndiyo sababu kuu inayoyahamakisha madola hayo ya kiistikbari na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana Iran kutokana na kupinga siasa za Marekani katika eneo hili, inafanyiwa vitisho vya kila namna na inawekewa vikwazo na mashinikizo kwani madola hayo yanajua kuwa Jamhuri ya Kiislamu inahatarisha manufaa ya siasa zao za kibeberu za kupenda kujikumbizia kila kitu upande wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, matokeo ya kutawala kambi ya kijahilia na madola ya kishetani ni kuenea maovu na utaghuti duniani na kuongeza kuwa: Pamoja na kwamba mrengo wa ujahilia na wa kitaghuti ulitumia bomu la atomiki kuua mamia ya maelfu ya watu huko Hiroshima (Japan) lakini baada ya kupita miaka mingi hadi leo hii unaendelea kufanya ukaidi na hautaki kuomba radhi kwa jinai yake hiyo kama ambavyo pia unaangamiza miundombinu ya nchi za Iraq na Afghanistan bila ya kujali chochote wala kujirudi moyoni.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe si mwanzishaji wa vita wala si mfanyaji wa harakati za kijeshi dhidi ya nchi yoyote ile lakini inasimamia na kulinda misimamo yake kwa sauti kubwa na itaendelea kufanya hivyo.
Ameashiria pia istilahi ilizokuwa zikitumiwa na Imam Khomeini (quddisa sirruh) kama vile fikra mgando kwa jina la Uislamu sambamba istilahi ya Uislamu wa Kimarekani na kuziweka istilahi hizo mbili katika mkabala wa istilahi ya Uislamu wa kweli na kuongeza kuwa: Makundi fasidi na yanayofanya ufisadi na uharibifu katika ardhi ambayo leo hii yanafanya jinai mbaya kabisa na ukatili wa kuchupa mipaka kwa jina la Uislamu, yanaungwa mkono na kusaidiwa kikamilifu na madola ya Magharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Wamagharibi wamejifanya kuunda muungano wa kupambana na Daesh (ISIS) lakini kwa hakika ni waungaji mkono wa genge hilo na wanafanya hivyo kwa makusudi ili kuendelea kuupiga vita Uislamu huku katika propaganda zao wakishikilia kutumia neno dola la Kiislamu kila wanapozungumzia kundi hilo kwa lengo la kuipaka matope sura ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia suala la kuenea na kuzidi kupata nguvu harakati ya Kiislamu licha ya kuweko vita hivyo vikubwa vya mrengo wa ujahilia dhidi ya Uislamu na kusema kuwa: Harakati ya Kiislamu ambayo ilipata nguvu na kuimarika baada ya kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran itaendelea na harakati zake na bila ya shaka yoyote itashinda tu.
Vile vile amesisitizia ulazima wa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutoogopeshwa na njama na vitisho vya madola ya kibeberu na kuongeza kuwa: Leo hii umma wote wa Kiislamu, iwe ni watu wa kawaida, au watu wenye vipawa au viongozi; kila mmoja ana jukumu - mbele ya harakati ya Kiislamu - la kukabiliana na mrengo huo wa ujahilia na kama kila mmoja atatekeleza majukumu hayo vizuri na kwa njia ipasayo basi atapata malipo na thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na mtu yeyote ambaye hatatekeleza vizuri majukumu yake, (hasara itakuwa kwake yeye mwenyewe lakini) harakati ya Kiislamu haitakwama bali itaendelea na njia yake, kwani hatima ya yote, ni Uislamu na Waislamu ndio watakaoshinda tu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmusilimia Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mab'ath ni siku ya rehema kwa viumbe wote na kuongeza kuwa: Rehema za Mtume wa Uislamu SAW si kwa ajili ya Waislamu tu, bali mtukufu huyo ni dhihirisho la rehema kwa wanadamu wote kwani ametumwa kuja kuwaonesha wanadamu wote njia ya uongofu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia tuhuma zinazotolewa leo hii duniani dhidi ya Uislamu kwa kuihusisha dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na vitendo vya kigaidi na ukatili na kusema kuwa: Wale watu ambao leo hii wameanzisha wimbi kubwa la vita dhidi ya Uislamu bila ya insafu, wanapaswa siku moja angalau wafanye uadilifu wa kuuangalia Uislamu kwa jicho zuri ili waweze kupata funzo kutokana na uadilifu uliofanywa na Mtume Muhammad SAW kwa washirika na watu waliokuwa wanakana kuwepo Mwenyezi Mungu.
Rais Hassan Rouhani ameongeza kuwa: Kwa upande mmoja, leo hii kuna vita na chuki za Wamagharibi ambao kwa karne nyingine wamekuwa wakiendesha propaganda dhidi ya Uislamu na kwa upande mwingine kuna marafiki wajinga au mamluki wanaotumiwa vibaya na Wamagharibi na kwa hakika hizo ni pande mbili za makali za mkasi unaolichana jina zuri la Uislamu.
Rais Hassan Rouhani aidha ameuliza swali akisema, ni nani aliyeleta ugaidi na ukosefu wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati na kuanzisha utawala ghasibu na dhalimu (wa Kizayuni) miaka 70 iliyopita? Amesema: Chanzo cha ukosefu mkubwa wa amani, ugaidi na vita vya mara kwa mara vinavyojiri katika eneo la Mashariki ya Kati, ni utawala wa Kizayuni (wa Israel) unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu.
Vile vile ameashiria suala la kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na kuvamiwa Iraq pamoja na kuzushwa ukosefu wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa: Wahusika wa jinai zote hizo ni Wazayuni na Wamarekani.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema, lengo kuu na la mwisho la mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuleta amani na usalama katika kona zote za dunia na kuhoji kwa kusema: Tutaweza vipi kukaa kimya wakati wananchi wa Yemen kila leo wanashambuliwa kinyama kabisa na watu ambao wanajinadi kuwa ni wafawidhi na wahudumu wa Masjidul Haram?
Rais Rouhani amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaona fakhari - chini ya miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu - kuwatetea na kuwahami watu wanaochulumiwa na itaendelea kufanya hivyo katika siku za usoni. Amesema: Popote itakapolazimu, tutatekeleza amri za Amirijeshi wetu Mkuu katika kuwasaidia na kuwa pamoja na watu wanaodhulumiwa popote pale ulimwenguni.

3495199

Habari zinazohusiana
captcha