IQNA

Ukombozi wa Palestina

Ujumbe Haniyah Katika Siku ya Nakba: Hakuna shaka kuwa Israel itaangamizwa

9:32 - May 16, 2024
Habari ID: 3478831
IQNA-Ismail Haniyah, Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema bila shaka utawala wa Kizayuni wa Israel hatimaye utaondolewa katika maeneo yote ya Wapalestina.

Kiongozi huyo wa Hamas aliyasema hayo katika hotuba yake siku ya Jumatano kwa mnasaba wa kuadhimisha kumbukumbu ya jinai ya kuwatimua Wapalestina kutoka ardhi zao mwaka 1948 na kufuatiwa na kuasisiwa utawala haramu wa Israel. Siku hii inajulikana kama Nakba.

Haniyah amesisitiza kuwa: "Kuondolewa Israel katika ardhi yetu ni jambo lisiloepukika na limetajwa katika Qur'ani na pia ni ukweli wa kihistoria."

Amesema katika tukio la Nakba, Wazayuni walikusudia kuangamiza taifa la Palestina lakini leo bado watu wa Palestina wana nguvu na wako imara katika mapambano. 

Kiongozi huyo wa Palestina ameapa kwamba operesheni dhidi ya Israel ambayo iliendeshwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba ilikuwa ni "utangulizi wa ukombozi na uhuru."

Haniyah amesema utawala wa Kizayuni wa Isarel ulipata pigo katika operesheni hiyo na ili kujaribu kuficha fedheha ya kushindwa utawala huo sasa unatekeleza mauaji ya kimbari.

Kiongozi huyo wa Hamas alikuwa akizungumzia vita vya mauaji ya kimbari ambavyo utawala haramu wa Israel ulianzisha kufuatia operesheni ya Hamas ya Kimbunga cha Al-Aqsa, ambapo hadi sasa utawala huo katili umeua zaidi ya Wapalestina 35,170, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Kwingineko katika matamshi yake, kiongozi wa Hamas amepongeza operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran ya Aprili 14 dhidi ya utawala wa Israel.

Amesema: "Pia tunathamini sana kipigo kilichotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa adui Mzayuni."

Katika operesheni hiyo Iran ilivurumisha ndege zisizo na rubani na makombora zaidi ya 300 katika kambi za kijeshi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Shambulio hilo kubwa lililopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli, lilikuwa jibu kwa shambulio la kigaidi la Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus. Katika hujuma hiyo iliyokiuka sheria za kimataifa,  watu 13, wakiwemo washauri saba wa kijeshi wanaohudumu katika Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) waliuawa shahidi.

4216104

captcha