IQNA

Rais Ramaphosa: Hali ya Ghaza inakumbusha zama za mfumo wa Apartheid Afrika Kusini

18:02 - May 19, 2021
Habari ID: 3473925
TEHRAN (IQNA)- Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema hali katika Ukanda wa Ghaza inamkumbusha kuhusu hali ilivyokuwa katika nchi yake wakati wa utawala wa mfumo katili wa ubaguzi wa rangi maarufu kama Apartheid.

Katika mahojiano na kanali ya France25 ya Ufaransa, Ramaphosa amesema vitendo vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhdi ya Wapalestina vinaleta taswira ya yale yalikokuwa yakijiri wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Ramaphosa amesema kuwa, Afrika Kusini inawaunga mkono Wapalestina huku akitoa wito kwa pande zote husika kufanya mazungumzo kama yale yaliyofanyika Afrika Kusini miaka ya awali ya muongo wa 90.

Mapema wiki hii pia, katika barua yake ya wiki, Ramaphosa amesema taswira za wanaume, wanawake na watoto Wapalestina wakitimuliwa kutoka nyumba zao za kifamilia ambazo wameishi kwa vizazi ni taswira ambazo zinaibua kumbukumbu chungu za wazalengo wengi Afrika kusini ambao walilazimishwa kuondoka katika makazi yao na ardhi zao kuporwa. Amesema familia yake binafsi , na familia za wengi Afrika Kusini zilidhalilishwa na kuumizwa wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Rais wa Afrika Kusini amesema vitendo vya utawala wa Kizayuni wa Israel ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yanataka ukaliwaji ambavu ardhi za Palestina usitishwe ili Wapalestina wapate haki zao.

Tangu siku ya Jumatatu ya tarehe 10 Mei, jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel limeanzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo hadi sasa Wapalestina wasiopungua 220, wakiwemo watoto 63 wameshauawa shahidi kutokana na mashambulio hayo na wengine zaidi ya 1,500 wamejeruhiwa.

Katika kujibu uchokozi na jinai hizo za kinyama za utawala haramu wa Israel dhidi ya Gaza, makundi ya muqawama ya Palestina yamevurumisha mamia ya makombora kuelekea miji na vitongoji haramu vya utawala ghasibu wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unayoikalia kwa mabavu.

3972424

Habari zinazohusiana
captcha