IQNA

Maombolezo

Rais wa Watu: Maisha na urithi wa Ebrahim Raisi, ambaye alifafanua upya siasa

20:37 - May 21, 2024
Habari ID: 3478865
IQNA-Rais wa Iran Ebrahim Raeisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na maafisa wengine kadhaa walikufa shahidi baada ya helikopta yao kuanguka katika milima ya kaskazini-magharibi mwa Iran siku ya Jumapili Mei 19

Ajali hiyo ilitokea katika jimbo la Azerbaijan Mashariki baada ya Rais Raeisi na ujumbe alioandamana nao kurejea baada ya kuzindua mabwawa mawili ya maji kwenye mpaka na nchi jirani ya Jamhuri ya Azerbaijan.

Helikopta ililazimika kutua kwa shida kutokana na hali mbaya ya hewa - ikiwa ni pamoja na mvua kubwa na ukungu mnene - ambayo ilifanya iwe vigumu kwa timu za utafutaji na uokoaji kutekeleza operesheni ya uokoaji kwa wakati.

Mabaki ya helikopta hiyo yaligunduliwa na timu za uokoaji wa dharura alfajiri ya Jumatatu asubuhi katika misitu minene iliyo baina ya miji ya Varzaqan na Jolfa katika jimbo la Azerbaijan Mashariki.

Pir-Hossein Koulivand, mkuu wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran (IRCS), alitangaza katika hotuba ya televisheni kwamba hakuna dalili ya uhai iliyopatikana kwenye helikopta iliyoanguka, na hivyo kumaliza matumaini yote ya walionusurika.

Makala hii itaangazia kwa mukhtasari maisha yaliyojaa nuru ya Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi ambaye alikuwa maarufu kama rais wa watu.

Sayyid Ebrahim Raisi alizaliwa mnamo Desemba 14, 1960, katika mji wa Mashhad kaskazini-magharibi mwa Iran.

Idara ya Mahakama

Alipanda daraja na kuwa mmoja wa shakhsia muhimu wa kisiasa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akishikilia nyadhifa nyingi muhimu akiwemo mkuu wa Idara ya Mahakama.

Kuanzia 2004 hadi 2014, Raisi alihudumu kama naibu mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran na alijulikana kwa mtazamo wake wa haki na wa kutetea haki kibinadamu, ambao ulimvutia miongoni mwa wananchi kote Iran.

Mnamo 2014, aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu (Mwendesha Mashtaka Mkuu) wa Iran, nafasi ambayo alishikilia hadi 2016.

Kisha akawa Mfawidhi wa Haram Takatifu ya Imam Ridha (AS), Imam wa nane wa Waislamu wa madhehebu yShia, katika mji wake wa Mashhad. Akiwa msimamizi wa eneo hilo takatifu, alitimiza kazi ambazo hazikufanywa hapo awali hasa

Uteuzi wake mashuhuri zaidi ulikuja mnamo Machi 2019 wakati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alipomchagua kuongoza Idara ya Mahakama ya Iran.

Alimrithi Ayatullah Sadeqh Amoli Larijani, ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa Baraza la Kuainisiha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu.

Akiwa mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Raisi alianzisha kampeni iliyosifiwa sana dhidi ya ufisadi katika mfumo huo na pia kutunga sheria za kuwalinda wanawake dhidi ya unyanyasaji wa majumbani.

Umaarufu wake uliongezeka sana wakati wa wadhifa wake kama Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, umaarufu ambao ulipelekea apendekezwa kuwania nafasi ya rais wa nchi.

Ulingo wa siasa

Akiwa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu, Raisi alichaguliwa kama mjumbe wa Baraza la Waanazuoni Wataalamu kutoka jimbo la Khorasan Kusini na alichaguliwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa 2006.

Mnamo mwaka wa 2016, alikua naibu kiongozi wa Baraza la Wataalamu, chombo cha Kikatiba chenye jukumu la kumteua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Rais alikua maarufu sana nchini Iran na hata  katika ulimwengu wa Kiislamu ambapo mnamo 2017 alipogombea katika uchaguzi wa rais dhidi ya Rais wa wakati huo Hassan Rouhani.

Alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo baada ya Rouhani, ambaye alipata kura milioni 23.5 dhidi ya kura milioni 15.7 za Raisi.

Aliwania urais mara ya pili mnamo 2021 ambapo aliibuka mshindi na hivyo akachukua hatamu za uongozi wa nchi

Katika uchaguzi huo, Raisi alipata ushindi wa kishindo, kwa kupata kura milioni 17.9 kati ya milioni 28.9 zilizopigwa.

Utawala wake ulikuwa tofauti vipi?

Rais wa nane wa Iran alianza rasmi uongozi wake tarehe 3 Agosti 2021 wakati wa kipindi kigumu cha change la corona. Baada ya miezi michache tu alifankiwa kupunguza idadi ya vifo kwa corona huku Iran ikigeuka kuwa mzalishaji mkubwa wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Raisi alikumbana na changamoto zingine kubwa, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kiuchumi yaliyozidishwa na vikwazo vinavyoongozwa na Marekani na kuongezeka kwa mvutano na Washington.

Kampeni zake za uchaguzi zilijikita katika kupambana na ufisadi na kupunguza matatizo ya kiuchumi.

Baada ya kuchukua wadhifa huo, aliwasifu vijana kama rasilimali ya thamani zaidi ya Iran katika msukumo wa ustawi wa uchumi na hivyo akijitolea kushughulikia masuala yao ya msingi, kama vile ukosefu wa ajira.

Zaidi ya hayo, Rasi alisisitiza haja ya kurekebisha mfumo wa urasimu, kupambana na rushwa na hali ya urasimu, na kuahidi kupunguza mfumuko wa bei hadi kiwango cha tarakimu moja kwa kuongeza uzalishaji.

Aliunga mkono juhudi za kidiplomasia za kupunguza athari za vikwazo vya Magharibi na kuboresha maisha ya watu wa Iran.

Akiwa mkosoaji mkubwa wa uwepo wa Marekani katika eneo hilo na sera yake ya kuweka vikwazo kwa mataifa huru, Raisi aliapa "kutopoteza hata dakika moja" katika kukabiliana na vikwazo.

Rais wa Iran alitangaza kwamba kuondoa vikwazo vya "katili" itakuwa suala la "lazima" kwa utawala wake, kupitia diplomasia hai ya kiuchumi na sera ya urafiki wa ujirani.

Misimamo imara

Alipitisha msimamo thabiti na wa kitaalamu katika sera ya kigeni ya Iran, haswa katika mazungumzo na Marekani na mataifa yenye nguvu ya Ulaya ili kufufua makubaliano ya nyuklia ya 2015.

Muda wake wa uongozi ulishuhudia mazungumzo mapya ya kuokoa makubaliano ambayo yalikuwa yamevunjwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump. Lakini juhudi hizo ziligonga mwamba tena kutokana na ukaidi wa  Marekani juu ya kuondolewa kwa vikwazo.

Kuhusu bara la Afrika, Rais Raisi alisisitiza kuimarisha uhusiano na mataifa ya Afrika katika nyanja za kiuchumi na kibiashara. Ili kutekeleza sera hivyo kivitendo alitembelea nchi za Afrika katika safari ya kihistoria.

Ziara yake ya siku tatu mwezi Julai mwaka jana ilimpeleka Kenya, Uganda na Zimbabwe, na hivyo ikawa ya kwanza ya rais wa Iran barani Afrika baada ya miaka 11. Aidha mwezi Agosti alielekea Afrika Kusini kushiriki katika kikao cha nchi za BRIC.

Raisi aliyekuwa na umri wa miaka 63 aliaga dunia katika ajali ya helikopta alipokuwa ziarani katika jimbo la Mashariki mwa Azerbaijan, ambapo yeye na mwenzake wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, walizindua mabwawa mawili yaliyojengwa kwenye Mto Aras.

Katika salamu zake za rambirambi, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema  kwamba Rais Raisi hakujua uchovu na katika tukio hili chungu, taifa la Iran limempoteza mtumishi mwaminifu, mkweli na mwenye thamani kubwa. Amesema Raisi alitanguliza ustawi wa nchi na wananchi kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu.

 3488426

captcha