IQNA

Kadhia ya Palestina

Hamas yasema mapatano ya kusitisha vita ni matunda na mapambano ya miezi 15 huko Ghaza

16:44 - January 16, 2025
Habari ID: 3480062
IQNA-Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema kuwa, kulazimika utawala wa Kizayuni kukubali kusimamisha vita na kukomesha mauaji yake ya kimbari dhidi ya wananchi wa Ghaza, ni matunda ya Muqawama (mapambano ya Kiislamu) na kusimama imara wananchi wa ukanda huo kwa zaidi ya miezi 15.

Harakati hiyo imesema hayo usiku wa kuamkia leo Alkhamisi kufuatia kutangazwa mapatano ya kusimamisha vita na utawala ghasibu wa Israel. 

Sehemu moja ya taarifa ya HAMAS imesema: "Makubaliano ya kusitisha mapigano ni matunda ya kusimama imara wananchi wetu wapendwa wa Palestina na Muqawama wetu wa kishujaa kwenye Ukanda wa Ghaza katika kipindi cha miezi 15 iliyopita."

"Makubaliano ya kukomesha uvamizi wa Ghaza ni mafanikio na ushindi kwa watu wetu, kwa Muqawama wetu, kwa taifa letu na watu huru wa duniani"  imesema sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya HAMAS. 

Hamas pia imesema: Tunatoa shukurani zetu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa kambi ya Muqawama katika eneo hili zima kwa msaada wao kwetu katika kukabiliana na mauaji ya kimbari yaliyokuwa yanafanywa na Israel.

Aidha taarifa ya pamoja ya harakati ya Jihad al Islami ya Palestina na ofisi ya Hamas kwenye Ukanda wa Ghaza imesema: "Leo, wananchi wetu na Muqawama wetu, tumefikia makubaliano kwa heshima kubwa na kumlazimisha adui kusitisha mashambulizi yake na kuondoka Ghaza. 

Harakati hizo zimewakumbuka kwa wema watu wote waliouwa shahidi katika kukinusuru Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa na kusisitiza kuwa hazitasita kufanya juhudi zozote za kuwahudumia wananchi katika eneo hilo na kukabiliana vilivyo na changamoto zinazokuja.

3491476

Kishikizo: hamas mapatano gaza israel
captcha