IQNA

Waislamu Australia

Msikiti Mkubwa wa Sydney wawasilisha ombi la kuadhini kwa vipaza sauti

10:20 - April 07, 2025
Habari ID: 3480505
IQNA – Msikiti mmoja mkubwa nchini Australia umeomba rasmi ruhusa ya kuanza kutumia vipaza sauti kuadhini katika kitongoji cha Lakemba, jiji la Sydney.

Msikiti wa Ali Bin Abi Talib, unaojulikana zaidi kama Lakemba Mosque, umeomba idhini kutoka Halmashauri ya Canterbury-Bankstown ili kufunga vipaza sauti vinne kwenye mnara wake. Lengo ni kurusha adhana kwa muda wa dakika tano hadi kumi na tano kila Ijumaa kabla ya Sala ya Ijumaa.

Endapo ombi hilo litapitishwa, Msikiti wa Lakemba utakuwa wa kwanza jijini Sydney kuadhini kwa vipaza sauti mara moja kwa wiki.

Nyaraka za mipango zilizoambatanishwa na maombi hayo zinaeleza muktadha wa kidini wa eneo hilo, zikibainisha kuwa takribani asilimia 61.2 ya wakazi wa Lakemba wanajitambulisha kama Waislamu.

Nyaraka hizo zinasema:

“Katika eneo la Lakemba, adhana ni sauti ya kawaida na ya kutuliza kwa wakazi wengi, inayotambulika kama sehemu ya mpangilio wa maisha ya kila siku na inayochangia mshikamano na imani ya pamoja.”

Msikiti huo unapatikana katika eneo lenye wakazi wengi, linalojumuisha nyumba za familia moja, majengo ya makazi ya pamoja, na maeneo machache ya kibiashara. Kwa mujibu wa kanuni za mipango ya halmashauri, uwekaji wa vipaza sauti unaruhusiwa endapo idhini rasmi itatolewa.

Pia, nyaraka hizo zinafananisha adhana na desturi za Kikristo kwa kusema:

“Adhana ni wito wa sala unaofanana na milio ya kengele za makanisa siku ya Jumapili wakati wa misa.”

Katika eneo la biashara la kati la jiji la Sydney, makanisa kadhaa – ikiwemo Kanisa Kuu la kihistoria la St Mary’s Cathedral – hupiga kengele zao mara kwa mara, baadhi ya vipindi hivyo vikidumu hadi saa moja.

3492600

captcha