IQNA

“Ubaguzi wa Wazi”: Taharuki Katika Seneti ya Australia Baada ya Mbunge wa Mrengo Mkali Kuvaa Burka

10:49 - November 25, 2025
Habari ID: 3481565
IQNA – Seneta mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia nchini Australia, Pauline Hanson, ameibua hasira kali Jumatatu baada ya kuingia bungeni akiwa amevaa vazi la Waislamu la burka, kama sehemu ya juhudi zake za mara kwa mara za kutaka vazi hilo lipigwe marufuku kwa sababu eti wanaovaa hufunika uso wote hadharani.

Hanson alionekana akiwa amevalia vazi hilo muda mfupi baada ya kunyimwa ruhusa ya kuwasilisha muswada wa kupiga marufuku burka na mavazi mengine yanayofanana kote Australia. Hii ni mara ya pili kwa Hanson kuleta burka ndani ya ukumbi wa Seneti kama chombo cha kisiasa.

Mvutano ulianza mara moja alipoingia bungeni, na kusababisha kelele kutoka kwa wabunge wa pande zote. Kikao kilisitishwa baada ya Hanson kukataa kuvua vazi hilo.

“Yeye ni seneta wa kibaguzi, akionyesha ubaguzi wa wazi,” alisema Mehreen Faruqi, seneta wa chama cha Greens kutoka New South Wales. Aliongeza: “Mavazi yanaweza kuwa chaguo la wabunge, lakini ubaguzi hauwezi kuwa chaguo la Seneti … mtu anatakiwa kumkemea kwa hilo.”

Seneta Fatima Payman pia alilaani kitendo hicho, akikitaja kuwa “cha fedheha na cha aibu.” Alisema: “Anadharau dini, anawadharau Waislamu walioko nje … hili ni kinyume kabisa na katiba. Inapaswa kushughulikiwa mara moja kabla ya kuendelea.”

Viongozi kutoka vyama vikuu viwili walijiunga na ukosoaji huo. Penny Wong, kiongozi wa serikali ya chama cha Labor katika Seneti, alieleza kuwa kitendo cha Hanson “hakistahili hadhi ya mwanachama wa Seneti ya Australia” na kuwasilisha hoja ya kumsimamisha kwa kukataa kuvua vazi hilo. Baada ya Hanson kukataa kutii, kikao kiliahirishwa. Anne Ruston, naibu kiongozi wa Seneti upande wa upinzani, pia alilaani kitendo hicho.

Hanson, seneta kutoka Queensland, amejulikana kwa misimamo yake ya kupinga uhamiaji tangu miaka ya 1990 na mara kwa mara amekuwa akipiga kampeni dhidi ya mavazi ya Kiislamu. Mnamo mwaka 2017, aliwahi pia kuvaa burka bungeni akitetea marufuku ya kitaifa ya vazi hilo ambalo huvaliwa na baadhi ya Waislamu. Chama chake cha One Nation kwa sasa kina viti vinne katika Seneti, baada ya kupata viti viwili zaidi katika uchaguzi wa Mei, kutokana na kuongezeka kwa uungwaji mkono wa sera za mrengo mkali wa kupinga uhamiaji.

3495514

Kishikizo: australia waislamu
captcha