IQNA

Leo XIV ateuliwa kumrithi Papa Francis kama kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani

20:15 - May 09, 2025
Habari ID: 3480657
IQNA-Kardinali Robert Prevost ametangazwa kuwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki. Yeye ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani na kuchukua jina la papa Leo XIV.

Kanisa Katoliki limempata Kiongozi wake mpya, Papa Leo wa 14 atakayewaongoza Wakatoliki kote ulimwenguni. Kiongozi huyo amepatikana Alhamisi jioni baada ya uchaguzi uliofanywa na makadinali wapatao 133 kutoka mataifa 70.

Papa Leo XIV, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Robert Francis Prevost, alizaliwa huko Chicago Septemba 14, 1955. Prevost alisoma katika Umoja wa Kitheolojia wa Kikatoliki wa Chicago, akitunukiwa diploma ya theolojia.

Akiwa na umri wa miaka 27, alikwenda Roma kusomea sheria za kanuni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Thomas Aquinas (Angelicum). Mafunzo yake ya kidini yalimfikisha Peru kama mmishionari, na baadaye akafanikiwa kupata nyadhifa mbalimbali nchini Marekani na Peru.

Prevost aliongoza dayosisi ya Chiclayo huko Peru na alikuwa makamu wa pili wa rais wa mkutano wa maaskofu wa Peru.  Papa Francis alifahamiana naye katika nchi hiyo ya Amerika Kusini na mwaka 2023 akamteua kuwa mkuu wa Baraza la Maaskofu, na kumfanya kuwa kardinali.

Baraza la Maaskofu ni idara ya wahudumu wa  Kanisa Katoliki. Katika jukumu hilo, amehusika na uteuzi wa maaskofu duniani kote kwa miaka miwili iliyopita. Wakati huo huo, Prevost alikuwa rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini.

Papa Leo XIV anatajwa kuwa kiongozi mwenye msimamo wa kati anayejumuisha pande zote za Kanisa. Anaelekea kuwa na mtazamo wa maendeleo kwenye masuala ya kijamii kama uhamiaji na umasikini, lakini anadumisha msimamo wa wastani kwenye masuala ya maadili ya Katoliki.

3493002

Habari zinazohusiana
captcha