IQNA

Ayatullah Hamedani atoa wito wa kuhitimishwa njaa na mzingiro Gaza katika barua kwa Papa Leo

11:04 - July 25, 2025
Habari ID: 3480994
IQNA-Mmoja wa viongozi wa ngazi za juu kidini nchini Iran amemwandikia barua Papa Leo XIV akisema: "Mienendo ya kikatili na isiyo ya kibinadamu ya utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni pamoja na kuzuia kupelekwa chakula na mahitaji muhimu kwa watu wa Gaza ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kidini, kibinadamu, maadili na sheria za kimataifa."

Ayatullah Nouri Hamedani amesema katika barua hiyo kwamba: Mienendo hiyo sio tu inastahili kulaaniwa lakini pia kufuatiliwa na kuadhibiwa katika mahakama za kimataifa.

Sehemu moja ya barua ya Ayatullah Nouri Hamedani kwa Papa Leo XIV, kiongozi wa Wakatoliki duniani, ambayo iliwasilishwa na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vatican inasema: 

Kama unavyojua, utu wa mwanadamu, kwa maana ya heshima, utukufu, na thamani ya asili ya mwanadamu, ni miongoni mwa dhana za kimsingi katika dini za mbinguni. Dini zote za Kiibrahimu zimesisitiza hadhi ya juu ya mwanadamu na kumtambua kuwa kiumbe chenye thamani ya asili na uwezo mkubwa wa kiroho, aliyeumbwa haswa na Mwenyezi Mungu.

Barua hiyo imesema: Dini zote za Mungu zinathibitisha kanuni za usawa, uhuru, wajibu na haki za binadamu, na zinapinga vikali ubaguzi wa rangi, wa kikabila na kitabaka.

Ayatullah Hamedani amemwambia Papa wa Kanisa Katoliki kwamba: Ni dhahiri kwamba dini za mbinguni, licha ya tofauti zao katika imani, zinashirikiana katika kusisitiza hadhi ya asili ya mwanadamu. Hadhi hii sio msingi wa haki za binadamu pekee, bali pia ni msingi wa mienendo ya kimaadili na ya kiutu kati ya wafuasi wa dini mbalimbali. Amesisitiza kuwa: Katika dunia ambapo dhulma na ubaguzi vinaongezeka, kurejea kwenye kanuni hii ya pamoja kunaweza kuwa njia bora ya kuishi pamoja kwa amani na maelewano kati ya watu wa dini mbalimbali.

"Kama unavyojua, Gaza ni ardhi iliyozingirwa ambayo imekuwa nembo ya kudhulumiwa ubinadamu. Wakati huu walimwengu wakishuhudia vifo vya kila siku vya watoto, wanawake na wanaume wasio na hatia kutokana na njaa, kiu na ukosefu wa dawa, utawala wa Kizayuni wa Israel unasababisha maafa makubwa mno katika historia ya sasa kwa kuendeleza mzingiro wake kamili wa Gaza na kuzuia kuingia kwa chakula na misaada ya kibinadamu katika eneo hilo", imesema sehemu ya barua ya Ayatullah Nouri Hamedani.

Ameongeza kuwa: Mienendo hii inapingwa na kulaaniwa sio tu katika mtazamo wa kibinadamu, lakini pia kwa mtazamo wa kidini, maadili na sheria za kimataifa.

Ayatullah Hamedani amemwambia Papa Leo XIV kwamba: Uislamu ni dini ya rehma na ubinadamu na inalaani vikali kuwadhuru watu wasio na hatia, hasa watoto na wanawake. Katika mafundisho ya Isa Masih pia, kuwasaidia wenye njaa na wahitaji ni wajibu wa kiungu. Taurati pia inasisitiza sana uadilifu na kutenda wema kwa wengine. Hivyo, kwa mtazamo wa dini za mbinguni, kuwanyima watu chakula ni dhulma kubwa dhidi ya matakwa ya Mungu.

Amesisitiza kuwa: "Mienendo ya kikatili na isiyo ya kibinadamu ya utawala wa Kizayuni wa Israel ikiwa ni pamoja na kuzuia kupelekwa chakula na mahitaji muhimu kwa watu wa Gaza ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kidini, kibinadamu, maadili na sheria za kimataifa."

"Sasa ni wajibu wa watu wote huru, mashirika ya haki za binadamu, taasisi za kidini, na mataifa yote kupaza sauti dhidi ya uhalifu huu na kuwa sauti ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza" imesema sehemu ya barua ya Ayatullah Hamedani kwa Papa Leo.

Amesema: Inatarajiwa kwamba mheshimiwa na viongozi wengine wa kidini watachukua hatua madhubuti na zenye taathira za kuzuia aina hii ya jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na utawala wa Kizayuni.

3493977

Habari zinazohusiana
captcha