IQNA

Msikiti wa Liverpool unakabiliwa na uhaba wa nafasi, huduma za mazishi

17:17 - May 19, 2025
Habari ID: 3480705
IQNA-Msikiti mashuhuri jijini Liverpool nchini Uingereza unakumbwa na changamoto ya uhaba wa nafasi na miundombinu huku ukijitahidi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za mazishi ya Kiislamu kutoka kwa jamii za ndani na za mikoa jirani.

Msikiti wa Al-Rahma, ulioko Hatherley Street, Toxteth, unajulikana kama kitovu cha Waislamu wa Liverpool. Umekuwa mahali pa msingi kwa mazishi ya Kiislamu katika eneo hilo, ikiwemo familia zinazotoka miji jirani kama Rochdale, Wirral, St Helens, na Sefton.

Licha ya kuhudumia jamii inayokadiriwa kuwa na Waislamu zaidi ya 40,000, msikiti huo kwa sasa una chumba kimoja cha kuosha maiti na kitengo kimoja cha kuhifadhi maiti kwa baridi, hali inayozua wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kutosheleza mahitaji ya kidini kwa waombolezaji.

Ibada ya Ghusl Mayyit, yaani kuosha mwili wa marehemu kabla ya mazishi, ni desturi muhimu katika Uislamu. Hatua hii, inayojumuisha kuosha mwili kwa sabuni na maji kisha kuufunika kwa sanda nyeupe, kwa kawaida hufanyika ndani ya masaa 24 baada ya kifo, na inachukuliwa kuwa wajibu wa kidini wa kijamii.

Kufikia Aprili 2023, Msikiti wa Al-Rahma ulikuwa umeshafanya mazishi ya Kiislamu 138, lakini miundombinu iliyopo inaelezwa kuwa imejaa kupita kiasi, haina faragha ya kutosha, na haifai kikamilifu kusaidia mahitaji ya kihisia ya familia za waombolezaji.

"Tunacho chumba kimoja tu cha kuosha maiti na friji moja la kuhifadhi miili. Hicho ndicho tulicho nacho. Kwa idadi ya Waislamu katika eneo hili, hakitoshi kabisa," alisema Abdulwase Sufian, mkurugenzi wa mazishi wa msikiti huo, alipoongea na Liverpool Echo.

Kutokuwepo kwa sehemu maalum ya mazishi kunalazimisha wafanyakazi wa msikiti mara nyingi kutumia vyumba vingine kwa ajili ya familia za waombolezaji, jambo ambalo linaweza kuathiri shughuli nyingine za kidini na kuongeza mzigo kwa miundombinu iliyopo, alisema Sufian.

Mpango wa kuboresha miundombinu ya msikiti sasa umeanza. Mradi uliopendekezwa, unaokadiriwa kugharimu zaidi ya pauni 100,000, unalenga kujenga chumba maalum cha Ghusl chenye nafasi ya kuhifadhi hadi miili mitano, chumba cha familia cha kutazama maiti, na ofisi ya msaada wa Janazah. Marekebisho haya yatafadhiliwa kupitia Sadaqah Jariyah, yaani michango ya hisani itakayomnufaisha mwenye kutoa hadi siku ya kiyama.

3493142

captcha