IQNA

Wizara ya Wakfu ya Misri kuandikisha watoto milioni moja kuhifadhi Qur'ani

15:08 - May 21, 2025
Habari ID: 3480715
IQNA – Msemaji wa Wizara ya Wakfu ya Misri ametangaza uzinduzi wa mpango wa majira ya kiangazi kwa watoto katika misikiti ya nchi hiyo.

Osama Raslan alisema kuwa kulingana na mpango huo, wizara imelenga kuandikisha watoto milioni moja katika masomo ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu na elimu ya kidini katika kipindi chote cha kiangazi.

Alisema wizara inalenga kuwashirikisha watoto milioni moja wa Misri katika misikiti kwa ajili ya kuhifadhi Kitabu Kitakatifu na kujifunza mafundisho ya kidini msimu huu wa kiangazi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Nile News cha Misri, aliongeza kuwa utekelezaji wa mpango wa kiangazi wa Qur'ani katika misikiti ulianza Mei 5 na utaendelea hadi Septemba 30.

Alisema kuwa misikiti iliyo katika mpango huo kote Misri, inayokadiriwa kuwa takriban 22,000, itakuwa mwenyeji wa programu hizo.

Alibainisha kuwa programu hizo zinafanyika kila Jumatatu na Jumatano baada ya sala ya alasiri.

Masomo ya kidini, programu za kuhifadhi Qur'ani, kuelewa maana ya aya za Qur'ani, na maelezo ya Hadithi ni sehemu ya programu za majira ya kiangazi, ambazo kupitia hizo, maadili ya kidini na ya kitaifa, pamoja na upendo kwa wengine, vitaimarishwa kwa kizazi kipya, alieleza.

Raslan aliendelea kusema kuwa programu nyingine maalum kwa watoto zilizokuwa zikiendeshwa katika mwaka mzima zilihitimishwa Mei 1.

3493164

captcha