IQNA

Iran kuandaa matukio ya kitaifa na kimataifa kuadhimisha miaka 1500 ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW)

17:48 - July 14, 2025
Habari ID: 3480944
IQNA – Mamlaka ya Iran imetangaza kuwa mfululizo wa matukio ya kitaifa na ya kimataifa yatafanyika kwa ajili ya kuadhimisha miaka 1500 tangu kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Rehema na Amani Zimshukie Yeye na Watu wa Nyumba Yake).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisheria, Kazem Gharibabadi, alisema Jumapili kuwa maadhimisho hayo yamefuatia kupitishwa kwa azimio lililowasilishwa na Iran katika mkutano wa hivi karibuni wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) uliofanyika Istanbul.

Kwa mujibu wa Gharibabadi, mawaziri wote walikubaliana kwa kauli moja kuidhinisha pendekezo la Iran la kuitangaza mwaka 1447 Hijria kuwa ni mwaka wa kihistoria unaoashiria kutimia kwa miaka 1500 tangu kuzaliwa kwa Mtume wa Mwisho, Muhammad Mustafa (SAW).

“Azimio hili linazihimiza nchi za Kiislamu kuendesha shughuli mbalimbali, kiutamaduni, kielimu, kitaaluma, kimedia, kibinadamu na kihisani, ili kuadhimisha tukio hili tukufu na kueneza ufahamu sahihi wa Uislamu na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW),” alieleza Gharibabadi.

Akaongeza kuwa azimio hilo linaangazia Uislamu kama dini ya amani, huruma na kustahamiliana. Pia linatambua mchango mkubwa wa ustaarabu wa Kiislamu kwa maendeleo ya binadamu na linahimiza mazungumzo ya kidini na uelewano baina ya dini tofauti.

“Mpango huu unahusisha uendeshaji wa matukio kadhaa ya kimataifa katika miji kama New York na Geneva, pamoja na jitihada za kuandikisha kumbukumbu hii kwenye kalenda rasmi ya UNESCO,” alisema.

Kazem Gharibabadi alisisitiza kuwa, kama taifa lililoanzisha mpango huu, Iran itakuwa mstari wa mbele katika uratibu na uendeshaji wa shughuli muhimu za kimataifa za kuadhimisha tukio hilo.

Naibu waziri huyo alitangaza kuwa matukio na programu mbalimbali zitazinduliwa hivi karibuni ndani ya Iran, na akatoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wananchi wa Iran kushiriki kikamilifu katika kusherehekea tukio hili la baraka kwa heshima na utukufu unaostahiki.

3493828

captcha