Dkt. Dauda Awwal amezindua kile anachokiita kuwa tafsiri ya kwanza kamili ya Qur’an Tukufu kwa lugha ya Kiyoruba na Kiingereza duniani.
Lugha ya Kiyoruba ni miongoni mwa lugha muhimu nchini Nigeria, na inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 16.
Mradi huo, unaoitwa “Global English-Yoruba Quran 4-in-1,” unajumuisha maandiko ya Qur’an kwa Kiarabu, tafsiri ya maneno kwa maneno kwa ajili ya matamshi sahihi (transliteration), tarjuma na tafsiri ya Kiyoruba kwa ustadi wa hali ya juu wa lugha, pamoja na tafsiri ya Kiingereza iliyoambatana na maelezo ya ziada, marejeo ya Hadith, mlinganisho wa kibiblia, na uchambuzi wa kielimu.
“Hii ni mara ya kwanza katika historia vipengele vyote hivi kuunganishwa katika Qur’an moja,” alisema Dkt. Awwal, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Muhammad Ibn Saud kilichopo Riyadh, Saudi Arabia.
“Kwa zaidi ya karne moja, Waislamu waongeao Kiyoruba wamekuwa hawana rejea kamili na ya kuaminika ya Qur’an kwa lugha yao. Mradi huu unakuja kuziba pengo hilo,” aliongeza.
Dkt. Awwal pia alitangaza uzinduzi wa toleo maalum kwa watoto liitwalo “Surah Zangu 13 za Kwanza kwa Watoto,” ambalo ni jumuisho lenye rangi, michoro, na mwingiliano, lililobuniwa mahsusi kwa watoto wa umri wa miaka mitano hadi kumi.
Toleo hilo la watoto linajumuisha tafsiri ya surah 13 fupi kwa Kiarabu, Kiyoruba, na Kiingereza, pamoja na michoro, maswali ya mazoezi, uhusiano na programu za simu, na pia visomo vya sauti na picha kwa ajili ya kusaidia elimu ya awali ya Kiislamu.
Mwanazuoni huyo ametangaza mpango wa kuchapisha na kusambaza nakala milioni tano za toleo la watoto bure katika mabara manne: milioni mbili barani Afrika, na milioni moja kila moja barani Ulaya, Asia, na Amerika. Pia, itatolewa katika njia za kidigitali kupitia programu na vitabu vya kielektroniki.
“Tunawaalika wafadhili kutoka duniani kote, taasisi za Kiislamu, na wahisani kushiriki nasi katika mradi huu wa kihistoria,” alisema Dkt. Awwal. “Hii siyo tu kitabu, bali ni urithi wa kitamaduni na daraja la maelewano baina ya dini mbalimbali.”
3494076