IQNA

Rais wa Nigeria: Qur'ani Tukufu ni Chanzo cha Nuru, Hekima na Faraja

11:50 - June 01, 2025
Habari ID: 3480770
IQNA – Rais wa Nigeria ameielezea Qur'ani Tukufu kama mwongozo kamili kwa wanadamu na chanzo cha nuru, hekima na faraja.

Rais Bola Ahmed Tinubu amewasihi Waislamu wa Nigeria kushikamana kwa dhati na mafundisho, maadili, na malengo matukufu ya Qur'ani Tukufu, ili Nigeria iweze kushuhudia na kufikia mafanikio makubwa.

Akizungumza katika kilele cha Mashindano ya Kuhifadhi na Kusoma Qur'ani yaliyoandaliwa kwa heshima ya marehemu mama yake, Abibatu Mogaji, huko Kano siku ya Jumamosi, hafla iliyoandaliwa na Seneta Bashir Lado, Rais huyo alisisitiza kuwa kitabu hicho kitakatifu ni mwongozo kamili kwa binadamu, chanzo cha nuru, hekima na faraja.

Akiwakilishwa na Msaidizi wake Maalum wa Masuala ya Kisiasa na mengineyo, Ibrahim Masari, Tinubu alisema:
“Mashindano haya ya kusoma Qur'ani si mashindano tu ya uhodari wa sauti, bali ni safari ya kiroho, ushahidi wa kujitolea, nidhamu na ibada ya kweli."

“Qur'ani ni neno la Mwenyezi Mungu, mwongozo kamili kwa wanadamu, chanzo cha nuru, hekima na faraja. Hivyo basi, kuna haja kwa Waislamu wote kuzingatia kwa makini mafundisho yake ili kubadili taswira ya jamii.”

“Nawasihi nyote kushikamana na mafundisho ya kitabu hiki kitukufu kwani hakika yatatuongoza katika kuishi kwa amani, maelewano na kuunda jamii yenye mafanikio, isiyo na chuki wala umwagaji damu.”

Tinubu aliendelea kusema:
“Tunaposhuhudia usomaji huu mzuri wa Qur'ani leo, tukumbuke ujumbe wa Qur'ani wa amani, umoja, haki na huruma. Tujitahidi kuendeleza mapenzi kwa kufuata mafundisho yake.”

3493293

 

Kishikizo: qurani tukufu nigeria
captcha