Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumapili alipowapokea viongozi na maelfu ya wananchi wa sekta mbalimbali hapa mjini Tehran, kwa mnasaba wa kumbukizi ya kuuawa shahidi Imam Ridha (SA) na kusisitiza kuwa, "Marekani inataka Iran iwe tiifu kwake. Taifa la Iran limechukizwa sana na tusi kubwa kama hilo na litasimama kwa nguvu zake zote dhidi ya wale ambao wana matarajio hayo ya njozi kutoka kwa wananchi wa Iran."
"Wale wanaotetea mazungumzo ya moja kwa moja na Washington kusuluhisha maswala yalipo wana mawazo duni," ameeleza bayana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Amebainisha kuwa, uadui wa Marekani dhidi ya Iran si jambo la hivi karibuni, kwani serikali mbalimbali za Marekani zimedumisha misimamo thabiti ya uadui, vikwazo na vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.
Hapo awali, sababu za uhasama huu mara nyingi zilifichwa kwa visingizio mbalimbali, kama vile ugaidi, haki za binadamu, masuala ya wanawake na demokrasia, Ayatuullah Khamenei amesema na kuongeza kuwa, "Utawala wa sasa wa Marekani umeweka wazi lengo lao halisi, kwani ulisema kuwa uhasama dhidi ya Iran unatokana na kutaka taifa hili liwe tiifu kwa matakwa ya Marekani.
Imam Khamenei amesisitiza haja ya kudumisha umoja wa kitaifa na kuwaunga mkono maafisa wa nchi hii ya Kiislamu, akionya kwamba, maadui wanataka kuleta migawanyiko baada ya kufeli kuishinda Iran kupitia vita.
Akijibu swali kuhusu sababu kuu ya uadui wa Marekani dhidi ya Iran, Ayatullah Khamenei amesema suala hilo linakwenda zaidi ya maelezo rahisi na limedumu kwa zaidi ya miongo minne chini ya tawala mtawalia za Marekani.
Amebainisha kuwa, Washington kwa muda mrefu imeficha uadui wake kwa visingizio kama vile ugaidi, haki za binadamu, masuala ya wanawake, au demokrasia, lakini rais wa sasa wa Marekani amefichua wazi sababu ya kweli.
Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amesema kulaaniwa kwa maneno na serikali za Magharibi hakutoshi na akahimiza hatua madhubuti za kukata aina zote za uungaji mkono kwa Israel.
Vile vile amesifu hatua za watu wa Yemen katika kukabiliana na Israel kama jibu "sahihi" na akasisitiza tena utayarifu wa Iran wa kuchukua hatua zozote zinazowezekana kwa ajili ya kuunga mkono kadhia hiyo.
3494372/