Ayatullah Khamenei ametoa matamshi hayo leo Jumanne, akihutubia wakuu wa mihimili mitatu ya dola ya serikali, mahakama, na bunge ya Jamhuri ya Kiislamu.
Hata hivyo, Kiongozi Muadamu alisema, “Hatujawa na matumaini makubwa kupita kiasi wala hatujawa na hali ya kukata tamaa kuhusu mazungumzo haya,” na akasisitiza, “Bila shaka, tuna shaka kubwa kuhusu upande wa pili.”
Kiongozi Muadamu amesisitiza kuwa: "Taratibu za kawaida za shughuli za nchi kwa ajili ya kufikia malengo yaliyowekwa katika nyanja zote lazima ziendelee kwa kasi kubwa zaidi; na kitu chochote kile kisifungamanishwe na matokeo ya mazungumzo."
Katika mkutano huo Ayatullah Khamenei amesema, ufuatiliaji wa masuala ni muhimu zaidi kuliko upitishaji maamuzi ya masuala hayo na akafafanua kwa kusema: "kuna sheria, kanuni na mipango mizuri nchini, lakini uhaba wa ufuatiliaji unakwamisha kufikiwa malengo kwa kiwango kinachokubalika".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, hamu, shauku na hamasa waliyonayo wakuu wa mihimili mitatu ya dola na maafisa wa vyombo mbalimbali ni ya kupongezwa, lakini haitoshi, na kwa sababu ya kukosekana ufuatiliaji unaohitajika, maamuzi na masisitizo ya viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali za uendeshaji yanakuwa dhaifu na katika masuala kadhaa huwa hayatekelezwi.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameyaelezea mazungumzo ya Oman kuwa ni moja ya makumi ya majukumu yanayotekelezwa na Wizara ya Mambo ya Nje na kusisitiza kuwa: masuala ya nchi yasifungamanishwe na mazungumzo hayo, na kosa lililofanywa katika JCPOA, la kufungamanisha masuala yote ya nchi na upigaji hatua wa mazungumzo hayo, halipasi kurudiwa tena.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya kuendelea shughuli za nchi katika nyanja zote za kiviwanda, kiuchumi, za ujenzi, za kiutamaduni na za utekelezaji wa miradi mikubwa na akasema: "hakuna hata moja kati ya masuala haya ambalo lina uhusiano wowote ule na mazungumzo ya Oman".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei akihutubia hadhara ya viongozi wakuu wa nchi
Sambamba na kuhadharisha juu ya "kufurutu mpaka katika kujenga matumaini au kupoteza matumaini" kuhusiana na matokeo ya mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: " katika hatua za kwanza imefanyika kazi nzuri kuhusu uamuzi wa nchi wa kufanya mazungumzo. Baada ya hatua hii pia inapasa zichukuliwe hatua kwa umakini, ikizingatiwa kuwa mistari myekundu ya upande wetu na ya upande wa pili inajulikana wazi".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "mazungumzo yanaweza kuwa na tija au yasiwe na tija. Na sisi pia hatuna mtazamo chanya wa kupita kiasi wala mtazamo hasi wa kupita kiasi kuhusu mazungumzo haya. Bila shaka, tuna mtazamo hasi wa kupita kiasi kwa upande wa pili (wa mazungumzo), lakini tuna mtazamo chanya kwa uwezo wetu wenyewe".
Ayatullah Khamenei pia amesisitiza umuhimu wa kupanua uhusiano na nchi jirani, vituo vya kiuchumi barani Asia na Afrika, pamoja na mataifa mengine, akihimiza juhudi za kuendelea kufuata mwelekeo huu.
Kwa kumalizia hotuba yake, Ayatullah Khamenei ameashiria jinai zisizo na kifani za genge la utendaji jinai la Kizayuni za kuwashambulia kwa makusudi wagonjwa, waandishi wa habari, magari ya kubebea wagonjwa, hospitali na watoto na wanawake madhulumu wa Ghaza na akasema: kutenda jinai kama hizo kunahitaji kuwa na ukatili na ushenzi usio wa kawaida, sifa ambazo genge hilo la utawala ghasibu limepambika nazo.
Aidha, amesema kuwepo harakati iliyoratibiwa kwa pamoja na Ulimwengu wa Kiislamu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na ikibidi za kioperesheni ni hitajio lenye uzito mkubwa na akaongeza kuwa: Bila shaka Mwenyezi Mungu atashusha mjeledi wake juu ya madhalimu hao, lakini hilo halipunguzi majukumu mazito ziliyonayo serikali na wananchi.
4276578