IQNA

Diplomasia

Ayatullah Khamenei akutana na Rais wa Cuba, ataka muungano wa kukabiliana na ubabe wa Marekani na Wamagharibi

18:55 - December 04, 2023
Habari ID: 3477987
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, uwezo mkubwa wa kisiasa na kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Cuba unapaswa kutumiwa kuunda muungano wa nchi ambazo zina misimamo sawa dhidi ya ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani na Wamagharibi.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo alasiri ya leo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba na ujumbe aliofuatana nao kuongeza kwamba, kuundwa muungano wa nchi ambazo zina misimamo sawa dhidi ya ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani na nchi za Magharibi, kwa kujikita zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi kunaweza kuwa na taahira kubwa katika kutatua masuala muhimu duniani kama kadhia ya Palestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu masuala ya Palestina: Kadhia ya Palestina haihusiani tu na matukio ya hivi karibuni ya Gaza na mashambulio ya mabomu, kwa sababu wananchi wa Palestina daima wamekuwa wakikabiliwa na mateso, masaibu na mauaji ya kila aina katika kipindi cha miaka 75 iliyopita, lakini sasa maafa katika Ukanda wa Gaza ni makubwa sana kiasi kwamba, ukweli halisi wa hilo uko wazi sasa mbele ya macho ya walimwengu na hakuna njia ya kuuficha.

Ayatullah Khamenei ameitaja misimamo ya Rais wa Cuba katika masuala ya kimataifa hususan suala la Palestina kuwa inakwenda sambamba na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu na kuashiria ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika vikao vya kimataifa na kuongeza kuwa, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unapaswa kuimarishwa zaidi katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ushirikiano katika uga wa kielimu.

4185888

captcha