IQNA

Ayatullah Khamenei: Iran katu haitafanya mazungumzo na madola ya kibabe

6:52 - March 09, 2025
Habari ID: 3480330
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyid Ali Khamenei, amesema kuwa sisitizo la baadhi ya madola ya kibabe juu ya kuandaa mazungumzo na Iran hakulengi kutatua matatizo.

Ayatullah Khamenei aliyasema haya katika mkutano na wakuu wa mihimili mitatu ya dola na maafisa wa mfumo mzima wa Iran jijini Tehran siku ya Jumamosi.

Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa: "Msisitizo wa baadhi ya serikali za kibabe juu ya mazungumzo si kwa ajili ya kutatua matatizo, bali ni njia ya kulazimisha matarajio yao binafsi."

Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitatimiza matarajio yao.

Aidha amesisitiza kuwa madola haya ya kibabe hayalengi tu kujadili suala la nyuklia, bali yanatumia mazungumzo kama "njia ya kuibua matarajio mapya" katika nyanja kama vile uwezo wa ulinzi wa Iran na uwezo wake wa kimataifa, mambo ambayo Iran haitakubali kamwe.

Kiongozi Muadhamu amebainisha kuwa madola hayo yanaibua suala la mazungumzo ili kushinikiza maoni ya umma, na ili wadia kuwa wako tayari kwa mazungumzo na kwamba eti  Iran ndiyo iliyokataa.

Ayatullah Khamenei pia amezikosoa nchi za Ulaya kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya Iran, akisema kwamba dai lao kuwa Iran haijatekeleza ahadi zake za nyuklia ni "lisilo la kimantiki."

Ayatullah Khamenei ameendelea kuzihutubu nchi za Ulaya hivi: "Mnasema Iran haijatekeleza ahadi zake za nyuklia. Vema, je, nyinyi mlitekeleza zenu? Hamkuzitimiza tangu mwanzo kabisa."

Kiongozi Muadhamu amebaini kuwa baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya 2015, nchi za Ulaya ziliahidi kufidia, lakini zilishindwa kutimiza ahadi yao.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa misingi ya ustaarabu wa Magharibi inapingana na misingi ya Uislamu na "hatuwezi kuwafuata."

Ameendelea kusema kuwa: "Tunaweza na tunapaswa kunufaika na chochote chenye manufaa popote pale duniani, lakini hatuwezi kutegemea misingi ya ustaarabu wa Magharibi."

Kiongozi Muadhamu amebaini kuwa kuwa matendo ya mataifa ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na ukoloni, uporaji wa rasilimali za mataifa mengine, mauaji ya halaiki, madai ya uongo kuhusu haki za binadamu na haki za wanawake, pamoja na viwango vyao vya undumakuwili katika masuala mbalimbali, vimeleta fedheha kwa ustaarabu wa Magharibi.

Ayatullah Khamenei amesema "[Dai la] uhuru wa maoni katika nchi za Magharibi si chochote zaidi ya uwongo.".

Kauli hiyo ya Kiongozi Muadhamu imekuja kufuatia madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba alikuwa amemtumia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei. 

Akizungumza na Fox News, Trump alisema alitarajia kufanikisha makubaliano na Tehran kabla ya kutoa vitisho vya kijeshi dhidi ya nchi hii.  Mtawala huyo wa Marekani ametishia kuwa kama mazungumzo hayatafanyika atachukua hatua kwa kusema: "Njia nyingine ni kuchukua hatua, kwa sababu huwezi kuruhusu silaha nyingine ya nyuklia." Iran imesisitiza mara kwa mara kwamba haijawahi kutafuta mpango wa kuunda silaha za nyuklia.

4270528

Habari zinazohusiana
captcha