Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amezungumzia kadhia ya Palestina ambapo amesema leo suala la Palestina limebadilika kuwa suala la kwanza linalozingatiwa na dunia nzima na kuwa muqawama wa wananchi wa Palestina umeuweka utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye njia ambayo mwisho wake si kingine isipokuwa kusambaratika na kutokomea kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika maadhimisho ya mwaka wa 35 wa kifo cha Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, kwamba tukio la kusikitisha na chungu la kumpoteza rais wa nchi na ujumbe aliokuwa ameandamana nao sio tu ni tukio kubwa ambalo limekuwa na taathira za ndani na kimataifa bali ni moja ya matukio muhimu ya historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema licha ya kutokea tukio hili chungu la kuondokewa na rais, lakini masuala ya nchi yamekuwa yakiendeshwa kwa utulivu na usalama kamili, suala linalothibitisha wazi uwezo mkubwa wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusimama imara wananchi na viongozi wa nchi katika misingi iliyowekwa na Hayati Imam Khomeini (MA).
Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza umuhimu wa kufanyika uchaguzi wa mapema kufuatia kifo cha rais wa nchi na kusema, hamasa ya uchaguzi huo itakamilisha hamasa ya kusindikizwa mashahidi watukufu wa serikali, na kuwa maadili yanapaswa kulindwa wakati wa kufanyika kampeni za uchaguzi. Katika miaka ya nyuma pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi mara nyingi wagombea wa uchaguzi wa rais kuepuka kubadilisha kampeni za uchaguzi kuwa uwanja wa vita vya kuwania madaraka na matusi ya kuvunjiana heshima, kama inavyofanyika katika kampeni za uchaguzi wa Marekani na baadhi ya nchi za Uaya.
Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu, uchaguzi ujao ni jambo lililojaa mafanikio, ambalo iwapo litafanyika vizuri na kwa njia inayofaa ya ushiriki mkubwa wa wananchi, bila shaka litaliletea matunda makubwa taifa la Iran. Awamu ya kumi na nne ya uchaguzi wa rais imepangwa kufanyika siku ya Ijumaa, Juni 28 kufuatia ajli mbaya ya helikopta iliyomuhusisha Sayyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ujumbe alioandamana nao, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Jumapili jioni (Mei 19) alipokuwa akirejea kutoka kwenye sherehe za ufunguzi wa mradi wa maendeleo kaskazini-magharibi mwa Iran, ambapo wote waliokuwa kwenye helikopta hiyo walikufa shahidi. Kwa mujibu wa kifungu cha 131 cha Katiba ya Iran, iwapo rais atakufa, kujiuzulu, kuwa mgonjwa kwa zaidi ya miezi miwili, kufutwa kazi au masuala mengine kama hayo, kaimu rais wa serikali ya mpito anawajibika kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kuandaa uchaguzi wa kuchaguliwa rais mpya ndani ya siku hamsini.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu nyingine ya hotuba yake katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu, amemtaja marehemu Imam kuwa shakhsia mwanamapambano na mwanafikra aliyekuwa na utambuzi mkubwa wa masuala ya Iran na dunia nzima na kuongeza kuwa, fikra za kisiasa za Imam Khomeini (MA) zilikuwa mwanzo wa mageuzi makubwa ambayo yaliweza kutambulisha uwezo wa kisiasa wa Uislamu kuwa ni nguvu kubwa ya kutegemewa na mataifa yaliyokuwa yakipigania mabadiliko na mageuzi.
3488612