Amesema Hijja inayoambatana na maarifa na mafunzo ni tiba ya maumivu ya leo ya ulimwengu wa Kiislamu. Ameashiria ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, na kusema kuwa jukumu muhimu zaidi la serikali za Kiislamu ni kuzuia kuendelea maafa ya kibinadamu huko Gaza na kuishinikiza Marekani ambayo ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala huo ghasibu kuacha kutoa misaada na uungaji mkono huo.
Matini kamili ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Sifa zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote, na swala na salamu zimwendee mbora wa viumbe wa Mwenyezi Mungu, Muhammad Al-Mustafa na Ahlul Bait wake wema na Maswahaba zake wateule, na wale wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Kiyama.
Hija ni matarajio ya waumini, sikukuu ya wenye shauku na riziki ya kiroho kwa wenye saada. Na ikiwa itaambatana na maarifa kuhusu siri zake za kina huwa ni tiba ya maumivu makuu ya Umma wa Kiislamu, bali kwa wanadamu wote.
Safari ya Hijja si kama safari nyingine zinazofanywa kwa ajili ya biashara au utalii au malengo mengine mbalimbali, ambapo ndani yake, baadhi ya ibada au amali njema pia hufanywa, bali safari ya Hajj ni zoezi la kuhama kutoka katika maisha ya kawaida kwenda kwenye maisha yanayofaa. Maisha yanayofaa ni maisha ya Tauhidi ambayo ndani yake kuna mzunguko wa kudumu unaozunguka mhimili wa ukweli, Sa'i ya kudumu katikati ya vilele vigumu, ramyi ya kudumu (kumpiga mawe shetani) dhidi ya shetani mwovu, wuquf (kisimamo) kinachoandamana na ukimya uliochanganyika na dhikri na dua, kumlisha maskini aliyekwama na mpita njia, kuzichukulia kuwa sawa rangi, jamii, lugha na jiografia ya wanadamu, na katika hali zote, kuwa tayari kwa ajili ya kutumikia, kumkimbilia Mwenyezi Mungu na kupeperusha bendera ya kutetea haki ni nguzo kuu na za kudumu za safari hii. Ibada ya Hajj inajumuisha mifano ya maisha haya na inafahamisha na kumwalika hujaji kweye maisha haya.
Mwaliko huu unapasa kusikika; moyo na macho ya nje na ya ndani yanapasa kufunguliwa. Mja anapasa kujifunza na kuwa na azma ya kunufaika na masomo haya. Kila mtu, anaweza kuchukua hatua kwenye njia hii kadiri ya uwezo wake; wakitangulia wanazuoni, wanafikra na wenye vyeo vya kisiasa na hadhi za kijamii.
Ulimwengu wa Kiislamu unahitaji kutumia mafunzo haya kuliko wakati mwingine wowote. Huu ni msimu wa pili wa Hijja, ambao unasadifiana na maafa ya Gaza na Asia Magharibi. Genge la jinai la Kizayuni linalotawala Palestina limefikisha maafa ya Gaza katika nukta isiyotasawurika kutokana na ukatili wake wa kutisha na unyama usio na mfano wake. Hivi sasa, watoto wa Kipalestina wanauawa kwa kiu na njaa, zaidi ya mabomu, risasi, na makombora; familia zinazoomboleza zinazidi kuongezeka kila siku kutokana na misiba ya kuwapoteza wapendwa, vijana, baba na mama zao; je, ni nani anayepaswa kusimama dhidi ya maafa haya ya kibinadamu?
Bila shaka, serikali za Kiislamu ndizo zinazobeba dhima ya jukumu hili katika hatua ya kwanza, nao raia wanapasa kuziwajibisha serikali zao katika hatua ya pili. Huenda serikali za Kiislamu zikawa zinakabiliwa na tofauti za kisiasa kuhusu masuala mbalimbali, lakini hili halipasi kuzizuia kufikia makubaliano na kushirikiana katika maafa ya kutisha ya Gaza na kutetea kundi linalodhulumiwa zaidi leo duniani. Serikali za Kiislamu lazima zifunge njia zote za misaada kuufikia utawala wa Kizayuni na kumzuia mtendajinai huyo kuendelea na tabia yake ya kinyama huko Gaza. Marekani ni mshirika wa moja kwa moja katika jinai za utawala wa Kizayuni; Washirika wa Marekani katika eneo hili na maeneo mengine ya Kiislamu wanapaswa kuzingatia wito wa Qur'ani wa kuwatetea wanaodhulumiwa na kuilazimisha serikali ya kiburi ya Marekani kuachana na tabia hiyo ya kidhalimu. Ibada ya kujibari (kujitenga) na maadui wakati wa Hajj ni hatua katika mwelekeo huu.
Muqawama wa kumiujiza wa watu wa Gaza umeliweka suala la Palestina katika kilele cha mazingatio ya ulimwengu wa Kiislamu na watu wote walio huru duniani. Fursa hii inapasa kutumika vizuri kwa ajili ya kuharakisha msaada kwa taifa hili linalodhulumiwa. Licha ya juhudi za mabeberu na waungaji mkono wa utawala ghasibu wa Kizayuni za kusahaulisha jina na kumbukumbu ya kadhia ya Palestina, lakini tabia ya shari ya viongozi wa utawala huo na siasa zao za kijinga zimeibua hali ambayo leo hii jina la Palestina linang'ara zaidi kuliko wakati mwingine wowote, ambapo chuki ya umma dhidi ya Wazayuni na waungaji mkono wao ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote; na hii ni fursa muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Wazungumzaji na wale walio katika nafasi nzuri za kijamii wanahitajika kuyafanya mataifa yao kuwa na ufahamu na mwamko zaidi na kupanua matakwa yanayohusiana na Palestina. Enyi mahujaji mliobahatika! Msighafilike na fursa hii ya kuomba dua na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati wa ibada ya Hijja, na mwombeni Mwenyezi Mungu Mtukufu ushindi dhidi ya madhalimu wa Kizayuni na waungaji mkono wao.
Swala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya mtukufu Mtume wa Uislamu na Aali zake watoharifu, na salamu pia ziwe juu ya Imam Mahdi, Baqiyatullah (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Sayyid Ali Khamenei
1404/3/9 (30/05/25)