IQNA

Syria Yazindua ‘Mushaf al-Sham’ Katika Maonesho ya Kimataifa ya Damascus

18:30 - September 05, 2025
Habari ID: 3481186
IQNA – Nakala maalum ya Qur’ani ya Kitaifa ya Syria, inayojulikana kama Mushaf al-Sham, imeonyeshwa rasmi katika banda la Wizara ya Wakfu wakati wa Maonesho ya 62 ya Kimataifa ya Damascus.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kiarabu la Syria (SANA), Mushaf al-Sham inachukuliwa kuwa nakala kubwa zaidi duniani ya Qur’ani iliyoandikwa kwa mkono. Mradi huu umechukua miaka 20 kukamilika.

Kazi hiyo ilianzishwa na mwanakaligrafia mashuhuri wa maandishi ya Kiarabu, Mohammad Moataz Obeid, ambaye alishirikiana na wanakaligrafia 62 kutoka nchi 17. Mushaf huo uliwasilishwa kwa mara ya kwanza kwa umma katika Maonesho ya Kimataifa ya Damascus yaliyofanyika kuanzia Agosti 28 hadi 31, tukio linalotambuliwa kama mojawapo ya matukio makubwa ya kiuchumi na kitamaduni nchini Syria.

Wazo la mradi huu lilianza mwaka 2005, Obeid aliponuia kuunda muswada wa kipekee wa Qur’ani unaoakisi thamani za kiroho na uzuri wa sanaa. Uandishi ulianza katika Khan Asaad Pasha, eneo la kihistoria katika mji wa zamani wa Damascus, ambako wachoraji wa kimataifa walikusanyika kwa maonesho maalum ya mradi huo.

Muswada huo ulikamilika ndani ya mwaka mmoja, na kurasa za awali ziliwasilishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2006 katika Ukumbi wa Kiti cha Enzi wa Ngome ya Aleppo. Mradi huu uliwaleta pamoja wasanii na wanakaligrafia kutoka Syria, Saudi Arabia, Uturuki, Palestina, Jordan, Kuwait, UAE, Yemen, Uholanzi, Pakistan, Bangladesh, Afghanistan, Misri, Iraq, Sudan, Libya, na Algeria – ishara ya mshikamano wa Umma wa Kiislamu.

Kila ukurasa wa Mushaf al-Sham una urefu wa mita 2.5 na upana wa mita 1.55. Qur’ani hiyo ina kurasa 125 kuu na kurasa 9 za nyongeza, kila moja ikiwa na mistari 33. Mapambo na urembo wa kurasa yalitekelezwa na msanii Abdul Karim Darwish, raia wa Syria mwenye asili ya Kijerumani.

Mnamo mwaka 2024, Qur’ani hiyo ilichapishwa kwa kutumia mbinu za kisasa na teknolojia ya hali ya juu. Obeid aliambia SANA kuwa muswada huo unawasilisha ujumbe wa amani na mapenzi kutoka Syria kwa ulimwengu mzima.

Wizara ya Wakfu ya Syria inapanga kuweka nakala ya kwanza katika Msikiti wa Umawi mjini Damascus, huku nakala nyingine zikitarajiwa kupelekwa katika Masjid al-Haram huko Makka, Al-Masjid al-Nabawi mjini Madina, na Msikiti wa Al-Aqsa katika al-Quds inayokaliwa kwa mabavu.

Kati ya mwaka 2006 hadi 2011, muswada huo ulipitia mapitio ya kitaaluma na ya kiisimu kabla ya kupata idhini rasmi kutoka Wizara ya Wakfu ya Syria na Baraza lake la Maulamaa. Baadaye ulithibitishwa na Wizara ya Wakfu ya Jordan mwaka 2012 na na taasisi ya Al-Azhar mwaka 2022.

Mradi huu umepelekwa kwa ajili ya kuingizwa katika Kitabu cha Rekodi za Dunia cha Guinness na unasubiri usajili rasmi chini ya nambari maalum ya rejea.

3494469

 

 

Kishikizo: msahafu syria
captcha