Katika mabara yote kutoka Ulaya hadi Australia na Amerika Kusini na Afrika, watu walikusanyika siku ya Alhamisi kupinga mzingiro wa jeshi la majini la Israel dhidi ya meli 41 zilizokuwa na angalau watu 400, wakiwemo watu mashuhuri kama mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg, na wanasiasa waliokuwa wakielekea Gaza, ambako Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa kuna hali ya njaa kali baada ya karibu miaka miwili ya vita vya mauaji ya halaiki vinavyoendeshwa na utawala wa Israel.
Huko Barcelona, takriban waandamanaji 15,000 walitembea wakipaza sauti: “Gaza, huko peke yako,” “Susia Israel,” na “Uhuru kwa Palestina.”
Televisheni ya Hispania ilionyesha polisi wa kutuliza ghasia wakitumia nguvu kuwazuia waandamanaji waliokuwa wakijaribu kuvuka vizuizi. Meya wa zamani wa Barcelona, Ada Colau, alikuwa miongoni mwa waliokamatwa baharini na sasa anakabiliwa na kufukuzwa nchini pamoja na wanaharakati wenzake, akiwemo mjukuu wa Nelson Mandela, “Mandla” Mandela.
Mamia ya waandamanaji pia walikusanyika nje ya bunge la Ireland huko Dublin, ambako mshikamano na Palestina mara nyingi huambatana na historia ya Ireland ya kupinga ukoloni wa Uingereza. Miriam McNally, ambaye binti yake alijiunga na msafara huo, aliambia AFP: “Nina wasiwasi mkubwa kwa ajili ya binti yangu, lakini najivunia sana kwa kile anachofanya. Anasimama kwa ajili ya ubinadamu mbele ya hatari kubwa.”
Paris ilishuhudia takriban waandamanaji 1,000 katika Place de la Republique, huku Marseille waandamanaji wapatao 100 wakikamatwa walipojaribu kuzuia ufikiaji wa Eurolinks, kampuni ya silaha inayoshutumiwa kwa kuuza vifaa vya kijeshi kwa Israel.
Huko Italia, ambapo vyama vikuu vya wafanyakazi vilitoa wito wa mgomo mkuu siku ya Ijumaa kuunga mkono msafara huo, maandamano yalienea katika miji mikuu. Roma pekee ilihusisha washiriki 10,000, kwa mujibu wa polisi, huku waandamanaji wakipaza sauti: “Tuko tayari kuzuia kila kitu. Mashine ya mauaji ya halaiki lazima isimame mara moja.”
Maandamano zaidi yalifanyika Berlin, The Hague, Tunis, Brasilia, Buenos Aires, Sydney, na Istanbul, ambako waandamanaji walitembea hadi ubalozi wa Israel wakiwa na mabango yaliyosema: “Zuio kamili dhidi ya uvamizi.”
Huko Brussels, takriban watu 3,000 walikusanyika nje ya Bunge la Ulaya, wakihimiza EU “ivunje mzingiro” huku kukiwa na moshi wa mabomu na fataki.
Hayo yanajiri wakati ambao vikosi katili vya Israel vinaendelea kushadidisha mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, vikisababisha vifo na majeraha kwa idadi kubwa ya watu, hususan katika maeneo ya kati na kusini mwa eneo hilo.
Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza siku ya Alhamisi kuwa angalau Wapalestina 66,225 wameuawa na wengine 168,938 kujeruhiwa katika vita vya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023.Wizara hiyo imebaini kuwa: “Waathirika wengi bado wamekwama chini ya vifusi na barabarani huku waokoaji wakishindwa kuwafikia".Wengi wa waliouawa shahidi ni wanawake na watoto.
3494849