IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jeshi la Majini la Iran limefanya kazi yenye kuleta fahari kubwa kwa taifa

21:06 - August 06, 2023
Habari ID: 3477391
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja kazi yenye mafanikio na fahari iliyofanywa na Kundi la 86 la Wanamaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuzunguka dunia nzima kuwa ni matokeo ya kazi ngumu, nia thabiti, kujiamini, uwezo wa kubuni, maarifa ya hali ya juu ya kijeshi, uongozi bora na "ujasiri na kusimama imara mkabala wa mashaka ya aina mbalimbali."

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo Jumapili katika kikao chake na makamanda wa Jeshi la Wanamaji, na wanajeshi wa Kundi la 86 la jeshi la majini na familia zao na kuongeza kuwa: Hatua hiyo kubwa kwa mara nyingine tena imedhihirisha kwamba mafanikio, maendeleo na matumaini yaliyotimia yamepatikana kutokana na harakati, bidii na kustahamili mashaka.

Ayatullah Khamenei amewashukuru kwa dhati makamanda na msafara wa Kundi 86, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji na wale wote walioshiriki katika kubuni, kusaidia na kutekeleza operesheni hiyo kubwa na kusema: "Harakati yenu hii leo ni matunda matamu ya hatua na juhudi za majeshi yote ya Iran katika miongo ya hivi karibuni katika sekta ya baharini, haswa kujitolea kwa mashahidi wa Jeshi la Wanamaji na familia zao, ambazo zinapaswa kupongezwa."

Amekutaja kusafiri baharini umbali wa kilomita elfu 65 ndani ya takriban miezi 8 kuwa ni fahari isiyo na kifani katika historia ya safari za baharini za Iran na akasema: Harakati hii yenye maana na ya kina haipaswi kuonekane kama tukio la kijeshi na la majini tu, kwa sababu kila moja ya vipengee vyake kinapaswa kupewa mazingatio na kuwa funzo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, safari ya baharini ya Kundi la 86 la Wanamaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeboresha sura ya kimataifa ya nchi.

Ameashiria baadhi ya vikwazo vinavyowekwa na Marekani katika sekta ya usafiri wa baharini na kusema: Ni makosa kusema kwamba, hawaruhusu meli fulani kupita katika baadhi ya meneo ya habarini, kwa sababu maji ya wazi ni ya wanadamu wote, na bahari na anga vinapaswa kuwa huru kwa mataifa yote; vivyo hivyo, usalama wa meli na usafirishaji wa baharini unapaswa kudhaminiwa kwa watu wote.

Ayatullah Ali Khamenei amesema: Leo hii Wamarekani wanashambulia meli za mafuta na kuyasaidia magenge ya magendo ya baharini katika eneo letu na maeneo mengine, jambo ambalo ni uvunjaji na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na za kibinadamu.

4160512

Habari zinazohusiana
captcha