IQNA

Idadi ya wanaoenda Umrah yaongezeka Jumada Al-Awwal

19:19 - November 28, 2025
Habari ID: 3481582
IQNA-Mamlaka ya Huduma za Msikiti Mtukufu wa Makka na Msikiti wa Mtume (SAW) jijini Madina imetangaza ongezeko kubwa la wageni katika mwezi wa Jumada Al-Awwal 1447 Hijria Qamaria, ambapo jumla ya watu milioni 66.6 walitembelea misikiti hiyo miwili mitukufu. Idadi hii imeongezeka kwa zaidi ya milioni 12 ikilinganishwa na kipindi kilichopita, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Saudi.

Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa waumini waliokusanyika katika Msikiti Mtukufu wa Makka (Masjid al Haram) walifikia takribani milioni 26, wakiwemo zaidi ya elfu 100 waliopata fursa ya kuswali ndani ya Hijr Ismail. Waliotekeleza Umrah walihesabiwa kufikia takribani milioni 14.

Msikiti wa Mtume (SAW) (Al Masjid An Nabawi) mjini Madina ulipokea zaidi ya waumini milioni 23.2, akiwemo zaidi ya laki 9 waliopata nafasi ya kuswali katika Al-Rawdah Al-Sharifah, na zaidi ya milioni 2.3 waliowasilisha salamu kwa Mtume (SAW) na maswahaba wake wawili.

Wizara ya Hija na Umrah, ikishirikiana na mamlaka husika, ilithibitisha kuwa idadi ya mahujaji wa Umrah ilihusisha wageni wa ndani na nje ya Ufalme, huku waliotoka nje wakifikia zaidi ya milioni 1.7.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, muda wa wastani wa kutekeleza ibada ya Umrah ulikuwa dakika 117; Tawaf dakika 43; Sa‘i kati ya Safa na Marwa dakika 49; kutoka viwanja hadi eneo la Mataf dakika 14; na kutoka Mataf hadi Sa‘i dakika 11.

Maafisa walisema maboresho ya kidijitali, uratibu wa vifaa na ufuatiliaji wa moja kwa moja vimewezesha harakati kuwa laini zaidi ndani ya Msikiti Mtukufu. Aidha, mifumo ya sensa katika milango mikuu inasaidia kufuatilia idadi ya waumini na kutoa mwongozo wa usimamizi wa umati kwa kushirikiana na taasisi husika.

3495535

Kishikizo: umrah
captcha